2 Wakorintho 13:8-14
2 Wakorintho 13:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli. Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini nyinyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu. Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa. Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa ishara ya upendo. Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni. Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.
2 Wakorintho 13:8-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana hatuwezi kutenda neno lo lote kinyume cha kweli, bali kwa ajili ya kweli. Maana twafurahi, iwapo sisi tu dhaifu, nanyi mmekuwa hodari. Tena twaomba hili nalo, kutimilika kwenu. Kwa sababu hiyo, naandika haya nisipokuwapo, ili, nikiwapo, nisiutumie ukali kwa kadiri ya uwezo ule niliopewa na Bwana, kwa kujenga wala si kwa kubomoa. Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa busu takatifu. Watakatifu wote wawasalimu. Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.
2 Wakorintho 13:8-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa maana hatuwezi kufanya lolote kinyume na kweli, bali kuithibitisha kweli tu. Tunafurahi wakati wowote tunapokuwa dhaifu, lakini ninyi mkawa na nguvu. Nayo maombi yetu ni kwamba mpate kuwa wakamilifu. Hii ndiyo sababu nawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana Isa aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa. Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, farijianeni, kuweni na nia moja, na mkae kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa busu takatifu. Watakatifu wote wanawasalimu. Neema ya Bwana Isa Al-Masihi, na upendo wa Mungu, na ushirika wa Roho wa Mungu ukae nanyi nyote.