2 Wakorintho 4:13-18
2 Wakorintho 4:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Maandiko Matakatifu yasema: “Niliamini, ndiyo maana nilinena.” Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena. Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. Yote haya ni kwa faida yenu, hata neema ya Mungu inapowafikia watu wengi zaidi na zaidi, shukrani nazo ziongezeke zaidi, kwa utukufu wa Mungu. Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
2 Wakorintho 4:13-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema, kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake. Haya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu. Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.
2 Wakorintho 4:13-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Niliamini, na kwa sababu hiyo nilinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda mfupi tu, yatuandalia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.
2 Wakorintho 4:13-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.