2 Wakorintho 4:7-12
2 Wakorintho 4:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa. Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu. Naam, muda tuishipo tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uhai wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa. Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi.
2 Wakorintho 4:7-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu. Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili kwamba uzima wa Yesu uweze kudhihirika katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti. Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.
2 Wakorintho 4:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twateseka, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twabeba katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu.
2 Wakorintho 4:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu.