Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 7:8-16

2 Wakorintho 7:8-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu. Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo. Basi, ijapokuwa naliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu. Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote. Kwa maana, ikiwa nimejisifu mbele yake katika neno lo lote kwa ajili yenu, sikutahayarishwa; bali, kama tulivyowaambia mambo yote kwa kweli, vivyo hivyo na kujisifu kwetu kwa Tito kulikuwa kweli. Na mapenzi yake kwenu yamekuwa mengi kupita kiasi, akumbukapo kutii kwenu ninyi nyote, jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu na kutetemeka. Nafurahi, kwa sababu katika kila neno nina moyo mkuu kwa ajili yenu.

2 Wakorintho 7:8-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Maana, hata kama kwa barua yangu ile nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda. Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru nyinyi kwa vyovyote. Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo. Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: Nyinyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Nyinyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili. Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu. Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo. Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia nyinyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli tupu. Hivyo upendo wake wa moyo kwenu nyinyi unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi nyinyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka. Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea nyinyi kabisa katika kila jambo.

2 Wakorintho 7:8-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa sababu, ijapokuwa niliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nilijuta, naona ya kwamba barua ile iliwahuzunisha, ingawa ni kwa muda tu. Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lolote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba iletayo wokovu isiyo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii gani ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo. Basi, ijapokuwa niliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali ili bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu. Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote. Kwa maana, ikiwa nimejisifu mbele yake katika neno lolote kwa ajili yenu, sikutahayarishwa; bali, kama tulivyowaambia mambo yote kwa kweli, vivyo hivyo na kujisifu kwetu kwa Tito kulikuwa kweli. Na mapenzi yake kwenu yamekuwa mengi kupita kiasi, akumbukapo kutii kwenu ninyi nyote, jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu na kutetemeka. Nafurahi, kwa sababu katika kila neno nina moyo mkuu kwa ajili yenu.

2 Wakorintho 7:8-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu, lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote. Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo. Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu. Kwa ajili ya haya tumefarijika. Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote. Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kila kitu tulichowaambia ninyi, kilikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia. Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, na kumpokea kwa hofu na kutetemeka. Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.