2 Wakorintho 9:1-9
2 Wakorintho 9:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma yenu hiyo kwa ajili ya watu wa Mungu. Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: “Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana.” Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi. Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema. Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika – bila kutaja aibu mtakayopata nyinyi wenyewe – kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi. Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ioneshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa. Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.” Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; wema wake wadumu milele.”
2 Wakorintho 9:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa habari za kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao. Lakini naliwatuma hao ndugu, ili kujisifu kwetu kwa ajili yenu kusibatilike katika jambo hili; mpate kuwa tayari, kama nilivyosema; kusudi, wakija Wamakedonia pamoja nami, na kuwakuta hamjawa tayari, tusije tukatahayarika sisi, (tusiseme ninyi), katika hali hiyo ya kutumaini. Basi naliona ya kuwa ni lazima niwaonye ndugu hawa watangulie kufika kwenu, na kutengeneza mapema karama yenu mliyoahidi tangu zamani, ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu. Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele.
2 Wakorintho 9:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhusu kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao. Lakini niliwatuma hao ndugu, ili kujisifu kwetu kwa ajili yenu kusibatilike katika jambo hili; mpate kuwa tayari, kama nilivyosema; kusudi, wakija Wamakedonia pamoja nami, na kuwakuta hamjawa tayari, tusije tukatahayarika sisi, (tusiseme ninyi), katika hali hiyo ya kutumaini. Basi niliona ya kuwa ni lazima niwaonye ndugu hawa watangulie kufika kwenu, na kutengeneza mapema karama yenu mliyoahidi tangu zamani, ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa nguvu. Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele.
2 Wakorintho 9:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hakuna haja yangu kuwaandikia kuhusu huduma hii itolewayo kwa ajili ya watakatifu. Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa watu wa Makedonia, nikiwaambia kuwa ninyi wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa. Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari. Kwa maana kama nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamjawa tayari, tutaona aibu kusema chochote juu yenu katika matoleo. Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu. Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. Kama ilivyoandikwa: “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele.”