2 Wafalme 16:10-20
2 Wafalme 16:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Ahazi alipokwenda Damasko kukutana na mfalme Tiglath-pileseri, aliona madhabahu huko. Basi, akamtumia kuhani Uria mfano kamili na mchoro wa madhabahu hiyo. Uria akajenga madhabahu hiyo kulingana na mfano huo na kuimaliza kabla ya Ahazi kurejea nyumbani. Ahazi aliporejea kutoka Damasko, aliiona hiyo madhabahu; basi akaikaribia madhabahu na kutoa sadaka juu yake. Alitoa sadaka yake ya kuteketezwa, ya nafaka, na ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka ya amani. Madhabahu ya shaba ambayo iliwekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, aliiondoa mbele ya nyumba kutoka nafasi yake katikati ya madhabahu yake na nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka kwenye nafasi iliyokuwa upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Kisha alimwamuru Uria, “Tumia hii madhabahu yangu kubwa kwa kuteketeza sadaka za asubuhi na sadaka za nafaka za jioni, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka za mfalme na za watu wote na pia sadaka za divai za watu. Irashie damu ya wanyama wote wa kuteketezwa ambao wametolewa sadaka. Lakini ile madhabahu ya shaba nitaitumia mimi kwa kuuliza kauli ya Mungu.” Naye Uria akafuata maagizo ya mfalme. Mfalme Ahazi aliziondoa papi zilizokuwa zimesimamishwa huko, akaondoa birika lililoitwa bahari ambalo lilikuwa juu ya wale fahali kumi na wawili wa shaba na kuliweka juu ya msingi wa mawe. Nalo jukwaa lililotumika siku ya Sabato lililokuwa limejengwa ndani ya nyumba pamoja na kivutio cha nje, mfalme alivihamisha kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya mfalme wa Ashuru. Matendo mengine yote ya mfalme Ahazi yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda. Ahazi akafa na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi, naye Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 16:10-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote. Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski. Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake. Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu. Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za BWANA, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya BWANA, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie. Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi. Mfalme Ahazi akakata papi za vitako, akaliondoa lile birika juu yake; akaiteremsha ile bahari itoke juu ya ng'ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe. Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya BWANA, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru. Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 16:10-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote. Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski. Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake. Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu. Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za BWANA, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya BWANA, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake. Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie. Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi. Mfalme Ahazi akakata papi za matako, akaliondoa lile birika juu yake; akaitelemsha ile bahari itoke juu ya ng’ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe. Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya BWANA, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru. Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 16:10-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Mfalme Ahazi akaenda Dameski kukutana na Tiglath-Pileseri wa Ashuru. Akaona madhabahu huko Dameski, naye akamtumia Uria kuhani mchoro wa hayo madhabahu, pamoja na maelezo ya mpango kamili wa ujenzi wake. Kwa hiyo Uria kuhani akajenga madhabahu kulingana na mipango yote ambayo Mfalme Ahazi alikuwa ameituma kutoka Dameski, na akamaliza ujenzi kabla ya Mfalme Ahazi kurudi. Mfalme aliporudi kutoka Dameski na kuona hayo madhabahu, akayasogelea na kutoa sadaka juu yake. Akatoa sadaka yake ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, akamimina sadaka ya kinywaji na kunyunyizia damu ya sadaka zake za amani juu ya hayo madhabahu. Mfalme Ahazi akayaondoa madhabahu ya zamani ya shaba kutoka hapo mbele ya Hekalu la BWANA, yaliyokuwa yamesimama kati ya ingilio la Hekalu na hayo madhabahu mapya, naye akayaweka upande wa kaskazini mwa hayo madhabahu mapya. Ndipo Mfalme Ahazi akatoa amri zifuatazo kwa Uria kuhani: “Juu ya hayo madhabahu kubwa mapya, toa sadaka ya asubuhi ya kuteketezwa na sadaka ya jioni ya nafaka, sadaka ya mfalme ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, pamoja na sadaka yao ya nafaka na sadaka yao ya kinywaji. Unyunyize juu ya hayo madhabahu damu yote ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu. Lakini mimi nitatumia hayo madhabahu ya zamani ya shaba kwa ajili ya kutafuta uongozi.” Naye Uria kuhani akafanya kama Mfalme Ahazi alivyoagiza. Mfalme Ahazi akaondoa mbao za pembeni na kuondoa masinia kwenye vile vishikilio vilivyohamishika. Akaondoa ile Bahari kutoka kwenye mafahali wa shaba walioishikilia, na kuiweka kwenye kitako cha jiwe. Kwa heshima ya mfalme wa Ashuru, akaliondoa pia pazia la Sabato lililokuwa limewekwa ndani ya Hekalu, na akaondoa ile njia ya kifalme ya kuingia kwenye Hekalu la BWANA. Matukio mengine ya utawala wa Ahazi na yale aliyoyafanya, je hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Ahazi akalala na baba zake, naye akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Hezekia mwanawe akawa mfalme baada yake.