Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 23:15-25

2 Wafalme 23:15-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Zaidi ya hayo aliharibu huko Betheli mahali pa kuabudia palipojengwa na mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi; aliharibu madhabahu hayo na kuvunja mawe yake katika vipandevipande, na kisha akaviponda mpaka vikawa vumbi; pia akachoma sanamu ya Ashera. Kisha Yosia alipogeuka aliona makaburi juu ya kilima; aliagiza mifupa ifukuliwe kutoka makaburini na kuichoma juu ya madhabahu; basi akayatia unajisi madhabahu sawasawa na neno la Mwenyezi-Mungu ambalo mtu wa Mungu alilitangaza, nabii ambaye alitabiri matukio haya. Halafu mfalme aliuliza, “Mnara ninaouona kule ni wa nini?” Nao watu wa mji wakamjibu, “Ni kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda na kutabiri mambo ambayo umeyafanya dhidi ya madhabahu pale Betheli.” Naye akaagiza, “Mwacheni hapo, mtu yeyote asiondoe mifupa yake.” Kwa hiyo waliiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya nabii aliyetoka Samaria. Katika kila mji wa Samaria mfalme Yosia aliharibu mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipojengwa na wafalme wa Israeli, ili kumkashifu Mwenyezi-Mungu. Madhabahu hayo yote aliyaharibu kama vile alivyofanya huko Betheli. Aliwaua makuhani wote wa miungu ya uongo juu ya madhabahu ambapo walitumikia na kuchoma mifupa yao juu ya madhabahu hayo. Kisha alirudi Yerusalemu. Kisha mfalme aliwaamuru watu wote, akisema, “Mfanyieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.” Hakuna Pasaka iliyosherehekewa kama hii tangu wakati wa waamuzi waliowaamua Waisraeli wala wakati wa ufalme wa Israeli au wa Yuda. Lakini, katika mwaka wa kumi na nane wa enzi ya Yosia, Pasaka ilisherehekewa kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu. Tena, ili mfalme Yosia atekeleze sheria zote zilizoandikwa katika kitabu alichokipata kuhani mkuu Hilkia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliondoa katika nchi ya Yuda na Yerusalemu, wachawi, watabiri, vinyago vya miungu, sanamu za miungu pamoja na vitu vyote vya kuchukiza. Kabla ya Yosia au baada yake hakuna mfalme yeyote aliyekuwa kama yeye, ambaye alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote, kwa nguvu zake zote na kwa roho yake yote kulingana na sheria ya Mose.

2 Wafalme 23:15-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena zaidi ya hayo, ile madhabahu iliyokuwako Betheli, na mahali pa juu alipopafanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli, madhabahu hiyo aliibomoa; na mahali pa juu alipateketeza, akapapondaponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera. Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la BWANA, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo. Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli. Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria. Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha BWANA, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli. Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu. Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni BWANA, Mungu wenu, Pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano. Hakika yake haikufanyika Pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda. Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika Pasaka hii kwa BWANA ndani ya Yerusalemu. Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya BWANA. Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea BWANA kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria ya Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.

2 Wafalme 23:15-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena zaidi ya hayo, ile madhabahu iliyokuwako Betheli, na mahali pa juu alipopafanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli, madhabahu hiyo aliibomoa; na mahali pa juu alipateketeza, akapaponda-ponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera. Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la BWANA, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo. Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli. Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria. Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha BWANA, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli. Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu. Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni BWANA, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano. Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda. Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa BWANA ndani ya Yerusalemu. Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya BWANA. Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea BWANA kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.

2 Wafalme 23:15-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hata madhabahu yaliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia miungu palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, alibomoa hata hayo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia miungu. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia miungu na kupasaga hadi pakawa vumbi, na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia. Kisha Yosia akatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa huko kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu ya Betheli ili kupanajisi. Hili lilitokea kulingana na neno la BWANA lililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya. Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?” Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu aliyekuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya hii madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.” Akasema, “Liacheni, msiliguse. Msimruhusu mtu yeyote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii ambaye alikuwa amekuja kutoka Samaria. Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa na kunajisi mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu ambapo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria, ambayo ilikuwa imemghadhibisha BWANA. Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika madhabahu zao wenyewe, na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu. Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwa BWANA Mungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.” Hapakuwahi kuwepo na adhimisho lingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za Waamuzi walioongoza Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda. Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwa BWANA huko Yerusalemu. Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa waaguzi, wanaoabudu mizimu, sanamu za kuagulia, sanamu za kuabudiwa, na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana huko Yuda na Yerusalemu. Aliyafanya haya ili kutimiza matakwa ya sheria iliyoandikwa ndani ya kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikipata ndani ya Hekalu la BWANA. Kabla wala baada ya Mfalme Yosia hapakuwepo na mfalme mwingine yeyote ambaye alimpenda BWANA kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria yote ya Mose.