2 Samueli 14:1-17
2 Samueli 14:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Yoabu mwana wa Seruya, alitambua kwamba maelekeo ya moyo wa Daudi yalikuwa kwa Absalomu tu. Hivyo alituma watu huko Tekoa ili wamtafutie mwanamke mwenye hekima. Walipomleta, akamwambia, “Jisingizie unafanya matanga. Vaa nguo za kuomboleza, usijipake mafuta, ila ujifanye kama mwanamke ambaye amekuwa katika maombolezo ya wafu kwa muda mrefu. Halafu nenda kwa mfalme ukamwambie yale ninayokuambia.” Kisha Yoabu akamwambia maneno ya kumwambia mfalme. Huyo mwanamke kutoka Tekoa akaenda kwa mfalme, akaanguka kifudifudi, mbele ya mfalme, akasujudu, akamwambia, “Ee mfalme, nisaidie.” Mfalme akamwambia, “Una shida gani?” Yule mwanamke akajibu, “Nasikitika, mimi ni mjane, mume wangu amekufa. Nilikuwa na watoto wa kiume wawili. Siku moja, walipokuwa mbugani, walianza kugombana. Kwa vile hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaamua, mmoja akampiga mwenzake, akamuua. Sasa ndugu zangu wote wamenigeuka mimi mtumishi wako; wanataka nimtoe kwao mtoto aliyemuua mwenzake ili wamuue kwa kuyaangamiza maisha ya ndugu yake. Hivyo, watamuua huyu ambaye sasa ndiye mrithi. Wakifanya hivyo, watazima kabisa tumaini langu lililobakia, na mume wangu hataachiwa jina wala mzawa duniani.” Mfalme akamwambia yule mwanamke, “Rudi nyumbani nitaamuru jambo lako liangaliwe.” Yule mwanamke kutoka Tekoa akasema, “Bwana wangu mfalme, hatia yote na iwe juu yangu na juu ya jamaa ya baba yangu. Hivyo, wewe na ufalme wako msiwe na hatia.” Mfalme akamwambia, “Mtu yeyote akikutishia mlete kwangu na hatakuja kukugusa tena.” Yule mwanamke akamwambia, “Tafadhali, mfalme, niombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili yule ndugu yangu ambaye angelipiza kisasi cha mauaji ya mwanangu asifanye hatia nyingine kubwa ya kumwua yule mtoto wangu mwingine.” Mfalme Daudi akamwambia, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utakaoanguka chini.” Yule mwanamke akamwambia, “Nakuomba, mimi mtumishi wako, uniruhusu niseme neno moja kwako mfalme.” Mfalme akamwambia, “Sema”. Yule mwanamke akamwambia, “Kwa nini basi, umepanga uovu huu dhidi ya watu wa Mungu? Kulingana na uamuzi wako juu ya jambo hilo wewe mwenyewe umejihukumu kuwa na hatia kwa sababu humruhusu mwanao arudi nyumbani kutoka alikokimbilia. Sisi sote lazima tutakufa. Sisi ni kama maji yaliyomwagika chini ambayo hayazoleki. Hata Mungu hafanyi tofauti kwa mtu huyu na tofauti kwa mwingine; yeye hutafuta njia ili waliopigwa marufuku, wakakimbia, wapate kurudi. Mimi nimekuja kuzungumza nawe, bwana wangu mfalme, kwani wamenitisha. Basi, mimi mtumishi wako, niliwaza kuwa, ‘Afadhali nikazungumze na mfalme, huenda akanitimizia mahitaji yangu mimi mtumishi wake. Maana mfalme atanisikiliza na kuniokoa mikononi mwa mtu ambaye anataka kuniangamiza mimi pamoja na mwanangu kutoka urithi wa Mungu’. Nami mjakazi wako nilifikiri kuwa, ‘Neno lake bwana wangu mfalme litanipa amani moyoni, kwani wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kupambanua mema na mabaya.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awe pamoja nawe.”
2 Samueli 14:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akatambua ya kuwa moyo wa mfalme unamwelekea Absalomu. Yoabu akatuma watu waende Tekoa, akaleta kutoka huko mwanamke mwenye akili, akamwambia, Nakusihi, ujifanye kama unaomboleza, ukavae nguo za kufiwa, nakusihi, wala usijitie mafuta, ila ukafanane na mwanamke aliyeomboleza siku nyingi kwa ajili yake aliyefariki; kisha uingie kwa mfalme ukamwambie maneno haya. Hivyo Yoabu akamtia maneno kinywani. Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifudifudi chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme. Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nilikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumwua mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala mabaki usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Yeyote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao. Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Maana kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa hamrudishi kwao tena yule mfukuzwa wake. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyoweza kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumishi wake. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumishi wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe.
2 Samueli 14:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akatambua ya kuwa moyo wa mfalme unamwelekea Absalomu. Yoabu akatuma watu waende Tekoa, akaleta kutoka huko mwanamke mwenye akili, akamwambia, Nakusihi, ujifanye kama unakaa matanga, ukavae nguo za kufiwa, nakusihi, wala usijitie mafuta, ila ukafanane na mwanamke aliyeomboleza siku nyingi kwa ajili yake aliyefariki; kisha uingie kwa mfalme ukamwambie maneno haya. Hivyo Yoabu akamtia maneno kinywani. Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifulifuli chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme. Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nalikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumfisha mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala masalio usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Ye yote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao. Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Kwani kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamleti kwao tena yule mfukuzwa wake. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumwa wake. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumwa wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe.
2 Samueli 14:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yoabu mwana wa Seruya akafahamu kuwa moyo wa mfalme ulikuwa na shauku ya kumwona Absalomu. Kwa hiyo Yoabu akamtuma mtu fulani kwenda Tekoa na kumleta mwanamke mwenye hekima kutoka huko. Akamwambia huyo mwanamke, “Jifanye uko katika maombolezo. Vaa nguo za kuomboleza, nawe usitumie mafuta yoyote ya uzuri, jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa na huzuni kwa siku nyingi kwa ajili ya kufiwa. Kisha nenda kwa mfalme ukazungumze maneno haya.” Naye Yoabu akaweka maneno kinywani mwa yule mwanamke. Huyo huyo mwanamke kutoka Tekoa alipofika kwa mfalme, akaanguka kifudifudi kumpa mfalme heshima, akasema, “Ee mfalme, nisaidie!” Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?” Akamwambia, “Mimi ni mjane hasa, mume wangu amekufa. Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwaamua. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua. Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake ambaye alimuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.” Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.” Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha enzi na asiwe na hatia.” Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.” Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe BWANA Mungu wake ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili kwamba mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama aishivyo BWANA, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.” Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.” Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali? Kama vile maji yaliyomwagika ardhini, yasivyoweza kuzoleka tena, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini Mungu haondoi uhai, badala yake, yeye hufanya njia ili kwamba aliyefukuzwa asibaki akiwa amefarikishwa naye. “Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba. Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka kwenye urithi Mungu aliotupatia.’ “Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. BWANA Mungu wako na awe pamoja nawe.’ ”