2 Samueli 14:18-33
2 Samueli 14:18-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo mfalme alipomjibu yule mwanamke, “Usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Yule mwanamke akasema, “Sema bwana wangu mfalme.” Mfalme akamwuliza, “Je, Yoabu anahusika katika jambo hili?” Yule mwanamke akasema, “Kama uishivyo, bwana wangu mfalme, mtu hawezi kukwepa kulia au kushoto kuhusu jambo ulilosema bwana wangu mfalme. Yoabu yule mtumishi wako ndiye aliyenituma. Ni yeye aliyeniambia maneno yote haya niliyokuambia mimi mtumishi wako. Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.” Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.” Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.” Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi. Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote. Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme. Absalomu alizaa watoto watatu wa kiume pamoja na binti mmoja jina lake Tamari. Tamari alikuwa mwanamke mzuri. Basi, Absalomu aliishi mjini Yerusalemu kwa muda wa miaka miwili mizima bila kumwona mfalme Daudi. Kisha, Absalomu alimtumia ujumbe Yoabu, ili aende kwa mfalme kwa niaba yake, lakini Yoabu akakataa. Absalomu akatuma ujumbe mara ya pili lakini Yoabu akakataa. Basi, Absalomu akawaambia watumishi wake, “Angalieni Yoabu ana shamba la shayiri karibu na langu. Nendeni mkalichome moto.” Kwa hiyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba la Yoabu. Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu akamwuliza, “Kwa nini watumishi wako wamechoma moto shamba langu?” Absalomu akamjibu, “Tazama, nilikupelekea ujumbe, uje huku ili nikutume kwa mfalme, ukamwulize: ‘Kwa nini niliondoka Geshuri? Ingekuwa bora kwangu kubaki huko’. Sasa nisaidie nipate kumwona mfalme. Kama nina hatia basi, na aniue!” Kwa hiyo Yoabu akaenda na kumweleza mfalme maneno hayo yote, naye akamwita Absalomu, naye akaingia kwa mfalme, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme. Na mfalme akambusu Absalomu.
2 Samueli 14:18-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lolote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme. Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kulia, au kwa kushoto, kukana neno lolote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumishi wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako; mtumishi wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu. Naye Yoabu akaanguka kifudifudi hadi chini, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako ninajua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumishi wake haja yake. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme. Ndipo Absalomu akatuma Yoabu aitwe, amtume kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja. Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba. Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu? Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, nikisema, Njoo kwangu, ili nikutume kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifudifudi hadi chini mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.
2 Samueli 14:18-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lo lote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme. Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kuume, au kwa kushoto, kukana neno lo lote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumwa wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako; mtumwa wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu. Naye Yoabu akaanguka kifulifuli hata nchi, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumwa wake haja yake. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme. Ndipo Absalomu akatuma kumwita Yoabu, ampeleke kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja. Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba. Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu? Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, kusema, Njoo kwangu, ili nikupeleke kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifulifuli hata nchi mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.
2 Samueli 14:18-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu kuhusu hilo nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.” Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako. Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, hufahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.” Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.” Yoabu akaanguka kifudifudi mpaka ardhini kumpa mfalme heshima, naye akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.” Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme. Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hapakuwa na kasoro. Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alikuwa akinyoa mara kwa mara zilipokuwa zinamwia nzito, alizipima uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme. Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura. Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme. Basi Absalomu akamwita Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamwita tena mara ya pili, lakini pia akakataa kuja. Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkalitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo. Basi Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?” Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!” ’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.” Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani akasujudu uso wake mpaka ardhini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.