2 Samueli 19:24-39
2 Samueli 19:24-39 Biblia Habari Njema (BHN)
Mefiboshethi mjukuu wa Shauli, alikwenda pia kumlaki mfalme Daudi. Tangu siku ile mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka aliporudi salama, Mefiboshethi alikuwa hajapata kuosha miguu yake, kukata ndevu zake na hakujali kufua nguo zake. Basi, ikawa alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, Daudi alimwuliza, “Je, Mefiboshethi, kwa nini hukuandamana pamoja nami?” Mefiboshethi akasema, “Ee bwana wangu mfalme, mtumishi wangu alinidanganya. Maana, mimi mtumishi wako, nilimwambia, ‘Nitandikie punda nipate kumpanda kwenda pamoja na mfalme,’ maana mimi mtumishi wako ni kilema. Sasa, amenisingizia kwako, ee bwana wangu mfalme. Lakini wewe, bwana wangu mfalme, uko kama malaika wa Mungu. Fanya lolote unaloona ni jema kwako. Maana, jamaa yote ya babu yangu walikuwa watu ambao wamestahili kuuawa mbele yako, bwana wangu mfalme. Lakini uliniweka mimi mtumishi wako miongoni mwa wale wanaokula mezani pako. Je, nina haki yoyote zaidi hata nikulilie mfalme?” Mfalme akamwambia, “Usiniambie zaidi juu ya mambo yako ya binafsi. Mimi nimekwisha amua kuwa wewe pamoja na Siba mtagawana nchi ya Shauli.” Lakini Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu Siba aichukue nchi yote peke yake. Mimi nimetosheka kwamba wewe bwana wangu mfalme umerudi nyumbani salama.” Barzilai Mgileadi alikuwa amefika kutoka Rogelimu. Alikuwa amekwenda pamoja na mfalme kwenye mto Yordani ili kumsindikiza hadi ngambo ya mto. Barzilai alikuwa mzee sana, mwenye umri wa miaka themanini. Naye Barzilai alikuwa amemtunza mfalme alipokaa huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Basi, mfalme Daudi akamwambia Barzilai, “Twende wote huko Yerusalemu nami nitakutunza.” Lakini Barzilai akamwambia mfalme, “Je, nina miaka mingi ya kuishi ndipo niende nawe mfalme mpaka Yerusalemu? Mimi leo nina umri wa miaka themanini. Je, nina uwezo wa kubainisha yaliyo mazuri na yale yasiyo mazuri? Je, mimi mtumishi wako, naweza kutambua ladha ya kile ninachokula au kunywa? Je, nitaweza kutambua uzuri wa sauti za waimbaji wanaume au wanawake? Kwa nini mimi mtumishi wako niwe mzigo wa ziada kwako, bwana wangu mfalme? Mimi mtumishi wako nitakwenda nawe mwendo mfupi ngambo ya Yordani. Kwa nini, mfalme anilipe zawadi kubwa hivyo? Nakuomba, uniruhusu mimi mtumishi wako, nifie katika mji wangu, karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini huyu mtumishi wako Kimhamu, mruhusu aende pamoja nawe bwana wangu mfalme, na mtendee yeye lolote unaloona ni jema.” Mfalme akamwambia, “Kimhamu atakwenda nami, na nitamtendea lolote lililo jema kwako. Na lolote utakalotaka nikutendee, nitakutendea.” Ndipo watu wote wakavuka mtoni Yordani na mfalme naye akavuka. Mfalme akambusu na kumbariki Barzilai, na Barzilai akarudi nyumbani kwake.
2 Samueli 19:24-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hadi siku hiyo aliporudi kwake kwa amani. Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi? Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumishi wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumishi wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumishi wako ni kiwete. Naye amenisingizia mimi mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako. Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumishi wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi? Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi. Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake. Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani. Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, alikuwa na umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa. Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu. Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Nina miaka mingapi ya kuishi, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu? Sasa nina miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumishi wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji wa kiume na wa kike? Kwa nini basi mtumishi wako azidi kumlemea bwana wangu mfalme? Mtumishi wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii? Niache nirudi basi, mimi mtumishi wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumishi wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako. Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako. Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarudi nyumbani kwake.
2 Samueli 19:24-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hata siku hiyo aliporudi kwake kwa amani. Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi? Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumwa wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumwa wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumwa wako ni kiwete. Naye amenisingizia mimi mtumwa wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako. Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumwa wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi? Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi. Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake. Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani. Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, amepata umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa. Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu. Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Siku ni ngapi za miaka ya maisha yangu, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu? Nimepata leo miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumwa wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji waume na wake? Kwa nini basi mtumwa wako amlemee bado bwana wangu mfalme? Mtumwa wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii? Niache nirudi basi, mimi mtumwa wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumwa wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako. Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako. Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarejea mahali pake.
2 Samueli 19:24-39 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Pia Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka kwenda kumlaki mfalme. Hakuwa amenawa miguu wala kunyoa ndevu zake wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka siku aliporudi ile salama. Wakati alipotoka Yerusalemu kuja kumlaki mfalme, mfalme akamuuliza, “Mefiboshethi, kwa nini hukufuatana nami?” Akasema, “Bwana wangu mfalme, maadamu mimi mtumishi wako ni kiwete, nilisema, ‘Nitandikiwe punda wangu, nimpande, ili niweze kwenda pamoja na mfalme.’ Lakini Siba mtumishi wangu akanisaliti. Naye amemchongea mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme. Bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu, kwa hiyo fanya lolote linalokupendeza. Wazao wote wa baba yangu hawastahili kitu kingine isipokuwa kifo kutoka kwa bwana wangu mfalme, lakini ulimpa mtumishi wako nafasi miongoni mwa wale waliokula mezani pako. Je, ninayo haki gani kumwomba mfalme zaidi ya hayo?” Mfalme akamwambia, “Kwa nini useme zaidi? Naamuru wewe na Siba mgawanye mashamba.” Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu achukue kila kitu, kwa kuwa sasa bwana wangu mfalme amerudi nyumbani salama.” Barzilai, Mgileadi, pia akashuka kutoka Rogelimu ili kuvuka Yordani pamoja na mfalme na kumsindikiza kutoka huko. Basi Barzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amempatia mfalme mahitaji wakati alipokuwa anaishi huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa mtu tajiri sana. Mfalme akamwambia Barzilai, “Vuka pamoja nami na ukae nami huko Yerusalemu, nami nitakupatia mahitaji yako.” Lakini Barzilai akamjibu mfalme, “Je, nitaishi miaka mingine mingapi, hata nipande kwenda Yerusalemu pamoja na mfalme? Sasa nina miaka themanini. Je, naweza kutofautisha kati ya lililo jema na lililo baya? Je, mtumishi wako anaweza kujua ladha ya kile anachokula au anachokunywa? Je, bado naweza kusikiliza sauti za waimbaji wa kiume na za wanawake? Kwa nini mtumishi wako aongeze mzigo kwa bwana wangu mfalme? Mtumishi wako atavuka Yordani pamoja na mfalme kwa umbali mfupi tu, lakini kwa nini mfalme anizawadie kwa namna hii? Mruhusu mtumishi wako arudi, ili mimi nikafie katika mji wangu mwenyewe karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini yupo hapa mtumishi wako Kimhamu. Mruhusu avuke pamoja na bwana wangu mfalme. Mtendee lolote linalokupendeza.” Mfalme akamwambia Barzilai, “Kimhamu atavuka Yordani pamoja nami, nami nitamtendea lolote litakalokupendeza. Nawe kitu chochote unachotaka kutoka kwangu nitakutendea.” Kwa hiyo watu wote wakavuka Yordani, kisha mfalme akavuka. Mfalme akambusu Barzilai na kumbariki; Barzilai akarudi nyumbani kwake.