2 Samueli 24:1-9
2 Samueli 24:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda. Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu. Naye Yoabu akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yo yote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli. Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kuume wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri; kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni, wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakatoka kusini kwa Yuda huko Beer-sheba. Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini. Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.
2 Samueli 24:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa mara nyingine, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia Waisraeli, akamchochea Daudi dhidi yao, akamwambia awahesabu watu wa Israeli na watu wa Yuda. Hivyo, mfalme akamwambia Yoabu, na makamanda wa jeshi waliokuwa pamoja naye, “Nendeni katika makabila yote ya Israeli kutoka Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu ili nipate kujua idadi yao.” Lakini Yoabu akamwambia mfalme, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa, nawe bwana wangu mfalme upate kuona ongezeko hilo kwa macho yako mwenyewe. Lakini, kwa nini wewe bwana wangu mfalme unapendezwa na jambo hili?” Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu na makamanda wa jeshi! Basi, Yoabu na makamanda wa jeshi wakaondoka mbele ya mfalme, wakaenda kuwahesabu Waisraeli. Walivuka mto Yordani wakianzia kuhesabu watu tangu Aroeri na mto ulioko bondeni kuelekea Gadi hadi Yazeri. Kisha, wakaenda Gileadi halafu Kadeshi katika nchi ya Wahiti, halafu wakawasili Dani na kutoka Dani wakazunguka kwenda Sidoni, na kufika kwenye ngome ya mji wa Tiro, wakaingia kwenye miji yote ya Wahivi na Wakanaani. Kisha, walitoka wakaenda Negebu ya Yuda huko Beer-sheba. Walipokwisha pitia katika nchi yote, walirejea Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Halafu Yoabu alimpelekea mfalme idadi ya watu. Katika Israeli kulikuwamo wanaume mashujaa 800,000 wenye ujuzi wa kutumia mapanga; na katika Yuda, kulikuwa na wanaume 500,000.
2 Samueli 24:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akamchochea Daudi juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu watu wa Israeli na Yuda. Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua idadi yao. Naye Yoabu akamwambia mfalme, BWANA, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yoyote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli. Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kulia wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri; kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni, wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakaenda katika Negebu ya Yuda huko Beer-sheba. Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa elfu mia nane wenye kufuta panga; nao wa Yuda walikuwa watu elfu mia tano.
2 Samueli 24:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hasira ya BWANA ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.” Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe watu wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.” Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “BWANA Mungu wako na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?” Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi, kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli. Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini ya mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri. Walikwenda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni. Kisha wakaenda kuelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walikwenda mpaka Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda. Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini. Yoabu akatoa hesabu ya wapiganaji kwa mfalme: Katika Israeli kulikuwako watu 800,000 wenye uwezo wa kupigana, na katika Yuda watu 500,000.