2 Samueli 24:10-17
2 Samueli 24:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Daudi alisumbuliwa sana rohoni mwake baada ya kuwahesabu watu. Kwa hiyo, Daudi akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo nililolifanya. Lakini sasa, ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.” Daudi alipoamka kesho yake asubuhi, wakati huo Mwenyezi-Mungu alimpa ujumbe nabii Gadi mwonaji wa mfalme Daudi, akisema, “Nenda ukamwambie hivi Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Ninakupa mambo matatu, nawe ujichagulie mojawapo, nami nitakutendea.’” Hivyo, Gadi akamwendea Daudi na kumweleza, akisema, “Je, wapendelea njaa ya miaka saba iijie nchi yako? Au je, wewe uwakimbie adui zako kwa miezi mitatu wanapokufuatia? Au kuwe na siku tatu ambapo nchi yako itakuwa na maradhi mabaya? Fikiri unipe jibu nitakalompa yeye aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nina mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu, kuliko kutiwa mikononi mwa watu, maana yeye ana huruma sana.” Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi, tangu asubuhi hadi wakati uliopangwa. Watu 70,000 walikufa nchini kote kutoka Dani mpaka Beer-sheba. Lakini wakati malaika aliponyosha mkono wake kuelekea mji wa Yerusalemu ili kuuangamiza, Mwenyezi-Mungu alibadilisha nia yake. Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo malaika aliyetekeleza maangamizi kwa watu, “Basi! Yatosha; rudisha mkono wako.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna, Myebusi. Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa anawaua watu, alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama, Mimi ndiye niliye na hatia! Mimi mwenyewe nimekosa! Hawa watu wapole hawakufanya uovu. Nakusihi sana uniadhibu mimi na jamaa ya baba yangu.”
2 Samueli 24:10-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia BWANA, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee BWANA, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la BWANA likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema, Nenda, ukanene na Daudi, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, BWANA akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa BWANA alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na BWANA, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.
2 Samueli 24:10-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia BWANA, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee BWANA, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.” Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la BWANA lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema: “Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ” Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa BWANA, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.” Basi BWANA akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi mpaka mwisho wa muda ulioamriwa, wakafa watu 70,000 kuanzia Dani hadi Beer-Sheba. Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, BWANA akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa BWANA alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna, Myebusi. Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia BWANA, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”
2 Samueli 24:10-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia BWANA, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee BWANA, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la BWANA likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, na kusema, Nenda, ukanene na Daudi, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Amua sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hadi wakati ulioamriwa; nao wakafa watu elfu sabini toka Dani mpaka Beer-sheba. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, BWANA akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa BWANA alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi, alipomwona malaika aliyewapiga watu, akanena na BWANA, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.