Matendo 1:4-11
Matendo 1:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
Matendo 1:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati alipokutana pamoja nao aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeni ile zawadi aliyoahidi Baba, ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je, Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?” Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni nyinyi, mtapokea nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.” Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena. Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mlivyomwona akienda mbinguni.”
Matendo 1:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kutoka kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na kote katika Yudea, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
Matendo 1:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?” Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.” Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena. Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”