Matendo 24:1-9
Matendo 24:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo. Paulo aliitwa, na Tertulo akafungua mashtaka hivi: “Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu. Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali. Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi. Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti. Tena alijaribu kulikufuru hekalu, nasi tukamtia nguvuni. [Tulitaka kumhukumu kufuatana na sheria yetu. Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu. Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo.” Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli.
Matendo 24:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akateremka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza mtawala habari za Paulo. Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa uongozi wako mambo mabaya yanasuluhishwa kwa ajili ya taifa hili, basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote. Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako. Kwa maana tumemwona mtu huyu kuwa mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazareti. Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu. Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu, Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwulizauliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi. Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo.
Matendo 24:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza liwali habari za Paulo. Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa maangalizi yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya taifa hili, basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote. Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako. Kwa maana tumemwona mtu huyu mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazorayo. Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu. Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu, Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwuliza-uliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi. Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo.
Matendo 24:1-9 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akateremka hadi Kaisaria pamoja na baadhi ya wazee na mwanasheria aitwaye Tertulo, wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala. Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na mabadiliko mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele. Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi. Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi. “Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanasiri, na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata. [Tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu. Lakini jemadari Lisia alitujia na nguvu nyingi, akamwondoa mikononi mwetu, akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kwa kumchunguza mwenyewe utaweza kujua ukweli kuhusu mashtaka haya yote tunayoleta dhidi yake.” Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka haya yote ni kweli.