Matendo 24:24-27
Matendo 24:24-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya siku chache, Felisi alifika pamoja na mkewe Drusila ambaye alikuwa Myahudi. Aliamuru Paulo aletwe, akamsikiliza akiongea juu ya kumwamini Yesu Kristo. Lakini wakati Paulo alipoanza kuongea juu ya uadilifu, juu ya kuwa na kiasi na juu ya siku ya hukumu inayokuja, Felisi aliogopa, akasema, “Kwa sasa unaweza kwenda; nitakuita tena nitakapopata nafasi.” Wakati huohuo alikuwa anatumaini kwamba Paulo angempa fedha. Kwa sababu hii alimwita Paulo mara kwa mara na kuzungumza naye. Baada ya miaka miwili, Porkio Festo alichukua nafasi ya Felisi, akawa mkuu wa mkoa. Kwa kuwa alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, Felisi alimwacha Paulo kizuizini.
Matendo 24:24-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya siku kadhaa, Feliki akafika pamoja na Drusila mkewe aliyekuwa Myahudi, akatuma kumwita Paulo akamsikiliza habari za imani iliyo kwa Kristo Yesu. Na Paulo alipokuwa akitoa hoja zake kuhusu haki, na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akaingiwa na hofu na kusema, Sasa nenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita. Pamoja na hayo alitaraji kwamba atapewa fedha na Paulo; kwa hiyo alimwita mara nyingi akaongea naye. Na miaka miwili ilipotimia, Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paulo akiwa amefungwa.
Matendo 24:24-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya siku kadha wa kadha, Feliki akafika pamoja na Drusila mkewe aliyekuwa Myahudi, akatuma kumwita Paulo akamsikiliza habari za imani iliyo kwa Kristo Yesu. Na Paulo alipokuwa akitoa hoja zake katika habari ya haki, na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akafanya hofu akajibu, Sasa enenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita. Pamoja na hayo alitaraji kwamba atapewa fedha na Paulo; kwa hiyo alimwita mara nyingi akaongea naye. Na miaka miwili ilipotimia, Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paulo amefungwa.
Matendo 24:24-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya siku kadhaa, Feliksi alikuja pamoja na Drusila mkewe, ambaye alikuwa Myahudi. Alituma aitiwe Paulo, naye akamsikiliza alipokuwa akinena juu ya imani katika Kristo Yesu. Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.” Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye. Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.