Matendo 25:1-12
Matendo 25:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku tatu baada ya kufika mkoani, Festo alitoka Kaisarea, akaenda Yerusalemu. Makuhani wakuu pamoja na viongozi wa Wayahudi walimpa habari kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Paulo. Walimsihi Festo awafanyie fadhili kwa kumleta Paulo Yerusalemu; walikuwa wamekula njama wamuue akiwa njiani. Lakini Festo alijibu, “Paulo atabaki kizuizini kule Kaisarea na mimi nitakwenda huko karibuni. Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu.” Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani. Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha. Kwa kujitetea, Paulo alisema, “Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu sheria ya Wayahudi, wala kuhusu hekalu, wala kumhusu Kaisari.” Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?” Paulo akajibu, “Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari, na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote. Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!” Basi, baada ya Festo kuzungumza na washauri wake, akamwambia Paulo, “Umekata rufani kwa Kaisari, basi, utakwenda kwa Kaisari.”
Matendo 25:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Festo alipokwisha kuingia katika mkoa, baada ya siku tatu akapanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. Kuhani Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi, na kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea na kumwua njiani. Lakini Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yuko tayari kwenda huko karibuni. Akasema, Wale walio na mamlaka kwenu na wateremke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko neno baya katika mtu huyu. Alipokwisha kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akateremkia Kaisaria; na siku ya pili akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe. Alipokuja, wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu naye wakaleta mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha. Paulo akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya hekalu, wala juu ya Kaisari. Lakini Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo? Paulo akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana. Basi ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka rufani kwa Kaisari. Basi Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari.
Matendo 25:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Festo alipokwisha kuingia katika uliwali, baada ya siku tatu akapanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. Kuhani Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi, na kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea na kumwua njiani. Lakini Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yu tayari kwenda huko karibu. Akasema, Wale walio na mamlaka kwenu na watelemke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko neno baya katika mtu huyu. Alipokwisha kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akatelemkia Kaisaria; hata siku ya pili akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe. Alipokuja, wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu yake wakaleta mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha. Paulo akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya hekalu, wala juu ya Kaisari. Lakini Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo? Paulo akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana. Basi ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka rufani kwa Kaisari. Basi Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari.
Matendo 25:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku tatu baada ya Festo kuwasili Kaisaria kuchukua wajibu wake mpya, alipanda kwenda Yerusalemu, ambako viongozi wa makuhani na viongozi wa Wayahudi walikuja mbele yake na kuleta mashtaka yao dhidi ya Paulo. Wakamsihi sana Festo, kama upendeleo kwao, aamuru Paulo ahamishiwe Yerusalemu, kwa kuwa walikuwa wanaandaa kumvizia ili wamuue akiwa njiani. Festo akawajibu, “Paulo amezuiliwa huko Kaisaria, nami mwenyewe ninakwenda huko hivi karibuni. Baadhi ya viongozi wenu wafuatane nami na kutoa mashtaka dhidi ya mtu huyo huko, kama amekosa jambo lolote.” Baada ya Festo kukaa miongoni mwao kwa karibu siku nane au kumi, akashuka kwenda Kaisaria na siku iliyofuata akaitisha mahakama, akaketi penye kiti chake cha hukumu, akaamuru Paulo aletwe mbele yake. Paulo alipotokea, wale Wayahudi waliokuwa wameteremka toka Yerusalemu wakasimama wakiwa wamemzunguka, wakileta mashtaka mengi mazito dhidi yake ambayo hawakuweza kuyathibitisha. Ndipo Paulo akajitetea, akasema, “Mimi sikufanya jambo lolote kinyume cha sheria ya Wayahudi au dhidi ya Hekalu au kinyume cha Kaisari.” Festo, akitaka kuwapendeza Wayahudi, akamuuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na kukabili mashtaka mbele yangu huko?” Paulo akasema, “Mimi sasa nimesimama mbele ya mahakama ya Kaisari, ambako ndiko ninakostahili kushtakiwa. Kama vile wewe mwenyewe ujuavyo vyema kabisa sijawatendea Wayahudi kosa lolote. Basi kama mimi nina hatia ya kutenda kosa lolote linalostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama mashtaka yaliyoletwa dhidi yangu na hawa Wayahudi si kweli, hakuna yeyote aliye na haki ya kunikabidhi mikononi mwao. Naomba rufaa kwa Kaisari!” Baada ya Festo kufanya shauri pamoja na baraza lake, akatangaza, “Wewe umeomba rufaa kwa Kaisari, nako kwa Kaisari utakwenda!”