Matendo 25:22-27
Matendo 25:22-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikia mtu huyo mimi mwenyewe.” Festo akamwambia, “Utamsikia kesho.” Hivyo, kesho yake, Agripa na Bernike walifika kwa shangwe katika ukumbi wa mkutano wakiwa wameandamana na wakuu wa majeshi na viongozi wa mji. Festo aliamuru Paulo aletwe ndani, kisha akasema, “Mfalme Agripa na wote mlioko hapa pamoja nasi! Hapa mbele yenu yuko mtu ambaye jumuiya yote ya Wayahudi hapa na kule Yerusalemu walinilalamikia wakipiga kelele kwamba hastahili kuishi tena. Lakini mimi sikuona kuwa alikuwa ametenda chochote kibaya hata astahili kupewa adhabu ya kifo. Lakini, kwa vile Paulo mwenyewe alikata rufani kwa Kaisari, niliamua kumpeleka. Kwa upande wangu sina habari kamili ambayo naweza kumwandikia Kaisari juu yake. Ndiyo maana nimemleta hapa mbele yenu na mbele yako mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza, niweze kuwa na la kuandika. Kwa maana nadhani itakuwa kichekesho kumpeleka mfungwa bila kutaja wazi mashtaka yanayomkabili.”
Matendo 25:22-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nilikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho. Kesho yake asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maofisa wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. Lakini mimi niliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nilikusudia kumpeleka kwake. Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuhojiwa nipate neno la kuandika. Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.
Matendo 25:22-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nalikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho. Hata asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maakida wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa. Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi. Lakini mimi naliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nalikusudia kumpeleka kwake. Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuulizwa-ulizwa nipate neno la kuandika. Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonyesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.
Matendo 25:22-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.” Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.” Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani. Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi. Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi. Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika. Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”