Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 28:1-10

Matendo 28:1-10 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Baada ya kufika nchi kavu salama, ndipo tukafahamu kwamba jina la kile kisiwa ni Malta. Wenyeji wa kile kisiwa walituonesha ukarimu usio wa kawaida. Waliwasha moto na kutukaribisha sisi sote kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa na baridi. Paulo alikusanya mzigo wa kuni, na alipokuwa anaweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu akatoka humo kwa ajili ya joto na kujisokotea mkononi mwake. Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akining’inia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni muuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.” Lakini Paulo akamkung’utia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yoyote. Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna chochote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu. Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la kiongozi mkuu wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio. Alitupokea kwake, na akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu. Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaugua homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya. Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa. Wakatupatia heshima nyingi, nasi tulipokuwa tayari kusafiri kwa meli, wakatupakilia vitu vyote tulivyokuwa tunavihitaji.

Shirikisha
Soma Matendo 28