Matendo 3:1-10
Matendo 3:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu. Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.
Matendo 3:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri. Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.
Matendo 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wakienda hekaluni, wakati wa sala. Wakati huo watu walikuwa wanambeba mtu mmoja kiwete tangu kuzaliwa. Watu hao walikuwa wakimweka huyo mtu kila siku kwenye mlango wa hekalu uitwao “Mlango Mzuri,” ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia hekaluni. Alipowaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni, aliwaomba wampe chochote. Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!” Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.
Matendo 3:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kulia, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu. Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango wa hekalu uitwao Mzuri; wakawa na mshangao na kustaajabia mambo yale yaliyompata.