Matendo 5:28-32
Matendo 5:28-32 Biblia Habari Njema (BHN)
“Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo cha mtu huyo.” Hapo Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, “Lazima tumtii Mungu, na siyo binadamu. Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya nyinyi kumuua kwa kumtundika msalabani. Huyu ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa kiongozi na Mwokozi, ili awawezeshe watu wa Israeli watubu, wapate kusamehewa dhambi zao. Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo.”
Matendo 5:28-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kulia, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wanaomtii.
Matendo 5:28-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.
Matendo 5:28-32 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.” Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Isa kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu wa Mungu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”