Matendo 9:1-9
Matendo 9:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa kuhani mkuu, akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia hiyo, awakamate na kuwaleta Yerusalemu. Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote. Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: “Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?” Naye Saulo akauliza, “Ni nani wewe Bwana?” Na ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya.” Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu. Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko. Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote.
Matendo 9:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, wanaume kwa wanawake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Wakati alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafla nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona wanitesa? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayemtesa. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, waliisikia sauti, lakini hawakuona mtu. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.
Matendo 9:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.
Matendo 9:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu, naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu. Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?” Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?” Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa. Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.” Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.