Amosi 7:1-9
Amosi 7:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA. Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukavila vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo aliyonionyesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake. BWANA akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe; na mahali palipoinuka pa Isaka patakuwa ukiwa, na mahali patakatifu pa Israeli pataharibika; nami nitaondoka nishindane na nyumba ya Yeroboamu kwa upanga.
Amosi 7:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena. Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema, “Haitakuwa hivyo!” Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema: “Hili pia halitatukia.” Mwenyezi-Mungu alinijalia tena maono mengine: Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama karibu na ukuta, ameshika mkononi mwake uzi wenye timazi. Naye akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nikamjibu, “Naona timazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema: “Tazama! Naweka timazi kati ya watu wangu Waisraeli. Sitavumilia tena maovu yao. Huko vilimani ambako wazawa wa Isaka hutambikia, kutafanywa kuwa uharibifu mtupu na maskani ya Waisraeli yatakuwa magofu. Nitaushambulia kwa vita ukoo wa mfalme Yeroboamu.”
Amosi 7:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ndiyo aliyonionesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA. Haya ndiyo aliyonionesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukaviteketeza vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo aliyonionesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake. BWANA akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe; na mahali palipoinuka pa Isaka patakuwa ukiwa, na mahali patakatifu pa Israeli pataharibika; nami nitaondoka nishindane na nyumba ya Yeroboamu kwa upanga.
Amosi 7:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ndilo alilonionyesha BWANA Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua. Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “BWANA Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!” Kwa hiyo BWANA akaghairi. Kisha BWANA akasema, “Hili halitatokea.” Hili ndilo BWANA Mwenyezi alilonionyesha katika maono: BWANA Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi. Ndipo nikalia, “BWANA Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!” Kwa hiyo BWANA akaghairi. BWANA Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.” Hili ndilo alilonionyesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake. Naye BWANA akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?” Nikamjibu, “Uzi wa timazi.” Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena. “Mahali pa Isaki pa juu pa kuabudia miungu pataangamizwa, na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa; kwa upanga wangu nitainuka dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”