Kumbukumbu la Sheria 29:14-29
Kumbukumbu la Sheria 29:14-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Wala sifanyi agano hili leo kwa niaba yenu tu na kutamka laana zake; sifanyi kwa niaba ya wale tu walio pamoja nasi leo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, bali pia kwa niaba ya wale ambao hawapo pamoja nasi leo. “Mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyosafiri katika nchi za mataifa mengine. Mliona sanamu zao za kuchukiza, miungu ya miti na mawe, ya fedha na dhahabu. Chukueni hadhari kwamba hakuna mwanamume, mwanamke, jamaa au kabila lolote linalosimama hapa leo litakalomwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwenda kutumikia miungu ya mataifa mengine. Jambo hili litakuwa kama mzizi utakaomea na kuzaa matunda machungu yenye sumu. Kama baada ya kusikia maneno ya agano hili ambayo mmeapishwa, halafu mtu akajiamini mwenyewe moyoni mwake na kusema atakuwa salama, hata kama atafuata ukaidi wake mwenyewe, hiyo itawaangamiza wote, wabaya na wema. Mwenyezi-Mungu hatasamehe mtu huyo, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu na wivu wake vitamwakia mtu huyo; laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamjia, naye Mwenyezi-Mungu atalifuta kabisa jina la mtu huyo kutoka duniani. Mwenyezi-Mungu atamtenga kutoka miongoni mwa makabila yote ya Israeli apatwe na maafa kufuatana na laana zote za agano zilizoandikwa katika kitabu hiki. Katika vizazi vijavyo, wazawa wenu na wageni kutoka nchi ya mbali wataona jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoiletea nchi hii maafa na mateso: Imejaa madini ya kiberiti na chumvi, imeteketea na kuwa tupu, haikupandwa mbegu na haioti chochote. Ni kama ilivyokuwa wakati Mwenyezi-Mungu alipoangamiza Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, kwa hasira yake kali. Naam, mataifa yote yatasema: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameitendea hivyo nchi hii? Hasira hii kubwa inamaanisha nini?’ Na jibu litatolewa: ‘Ni kwa sababu walivunja agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao ambalo alifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri, wakaenda kuitumikia na kuiabudu miungu mingine, ambayo hawakuijua hapo awali, wala Mwenyezi-Mungu hakuwa amewapa. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya nchi hii, na kuiletea laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. Naye Mwenyezi-Mungu, akawangoa kutoka katika nchi yao kwa hasira na ghadhabu kubwa, akawatupa katika nchi nyingine kama ilivyo leo.’ “Mambo ya siri ni ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini yale ambayo ameyafunua ni yetu na wazawa wetu milele, ili tutekeleze maneno yote ya sheria hii.”
Kumbukumbu la Sheria 29:14-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki; ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya BWANA, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo; (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao; nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;) asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache BWANA, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga; ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu; BWANA hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya BWANA na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na BWANA atalifuta jina lake chini ya mbingu. BWANA atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika kitabu hiki cha torati. Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia BWANA; ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua BWANA kwa ghadhabu yake na hasira zake; mataifa yote watasema, Mbona BWANA ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake joto la hasira hizi kubwa? Ndipo watakaposema watu, Ni kwa kuwa waliacha agano la BWANA, Mungu wa baba zao, alilofanya nao hapo alipowatoa katika nchi ya Misri; wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye; ndipo ikawashwa hasira ya BWANA juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki; BWANA akawang'oa katika nchi yao kwa hasira, na ghadhabu, na makamio makuu, akawatupa waende nchi nyingine, kama hivi leo. Mambo ya siri ni ya BWANA, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.
Kumbukumbu la Sheria 29:14-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki; ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya BWANA, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo; (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao; nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;) asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache BWANA, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga; ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu; BWANA hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya BWANA na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na BWANA atalifuta jina lake chini ya mbingu. BWANA atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika chuo hiki cha torati. Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia BWANA; ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua BWANA kwa ghadhabu yake na hasira zake; mataifa yote watasema, Mbona BWANA ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake hari ya hasira hizi kubwa? Ndipo watakaposema watu, Ni kwa kuwa waliacha agano la BWANA, Mungu wa baba zao, alilofanya nao hapo alipowatoa katika nchi ya Misri; wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye; ndipo ikawashwa hasira ya BWANA juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki; BWANA akawang’oa katika nchi yao kwa hasira, na ghadhabu, na makamio makuu, akawatupa waende nchi nyingine, kama hivi leo. Mambo ya siri ni ya BWANA, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.
Kumbukumbu la Sheria 29:14-29 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ninafanya agano hili pamoja na kiapo chake, sio na ninyi tu mnaosimama hapa na sisi leo mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali pia pamoja na wale ambao hawapo hapa leo. Ninyi wenyewe mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyopita katikati ya nchi hadi tukafika hapa. Mliona miongoni mwao machukizo yao, na sanamu za miti na mawe, za fedha na dhahabu. Hakikisheni kwamba hakuna mwanaume au mwanamke, ukoo au kabila miongoni mwenu leo ambalo moyo wake utamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwenda kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisheni hakuna mzizi miongoni mwenu unaotoa sumu chungu ya namna hii. Mtu wa namna hii asikiapo maneno ya kiapo hiki, hujibariki mwenyewe, na kisha hufikiri, “Nitakuwa salama, hata nikiendelea kuifuata njia yangu mwenyewe.” Hili litaleta maafa juu ya nchi iliyoneshewa sawasawa na nchi kame. Mwenyezi Mungu kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na Mwenyezi Mungu atafuta jina lake chini ya mbingu. Mwenyezi Mungu atamtwaa peke yake kutoka makabila ya Israeli kwa maangamizi, kulingana na laana zote za agano zilizoandikwa kwenye Kitabu hiki cha Torati. Watoto wako watakaofuata baada yako katika vizazi vya baadaye na wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali, wataona maafa, yaliyoipata nchi na magonjwa ambayo Mwenyezi Mungu aliyaleta juu yake. Nchi yote itakuwa jaa linaloungua la chumvi na kiberiti: hakutakuwa kilichopandwa, hakutakuwa kinachochipua, wala hakutakuwa na mimea inayoota juu yake. Itakuwa kama maangamizi ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambazo Mwenyezi Mungu aliangamiza kwa hasira kali. Mataifa yote yatauliza: “Kwa nini Mwenyezi Mungu ameifanya hivi nchi hii? Kwa nini hasira hii kali ikawaka?” Na jibu litakuwa: “Ni kwa sababu watu hawa waliacha agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, agano alilofanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri. Walienda zao na kuabudu miungu mingine na kuisujudia, miungu wasioijua, miungu ambayo Mungu hakuwapa. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya nchi hii, hivyo Mungu akaleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. Katika hasira kali na katika ghadhabu kuu Mwenyezi Mungu aliwang’oa kutoka nchi yao na kuwasukumia katika nchi nyingine, kama ilivyo sasa.” Mambo ya siri ni ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.