Mhubiri 4:9-12
Mhubiri 4:9-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Ni afadhali kuwa wawili kuliko mtu kuwa peke yake. Kwa sababu wawili watapata tuzo la kazi yao. Ikijatokea mmoja akaanguka, huyo mwenzake atamwinua. Lakini ole wake aliye peke yake akianguka! Huyo hatakuwa na mtu wa kumwinua! Hali kadhalika, wawili wakilala pamoja watapata joto; lakini mtu akiwa peke yake atajipatiaje joto? Mtu akiwa peke yake aweza kushindwa na adui, lakini wakiwa wawili watamkabili na kumshinda adui. Kamba tatu zikisokotwa pamoja hazikatiki kwa urahisi.
Mhubiri 4:9-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Kwa sababu wana tuzo njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kupata moto? Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watamstahimili; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.
Mhubiri 4:9-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.
Mhubiri 4:9-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao: Kama mmoja akianguka, mwenzake atamwinua. Lakini ni jambo la kuhuzunisha kwa mtu yule aangukaye naye hana wa kumwinua! Pia, kama wawili wakilala pamoja watapashana joto. Lakini ni vipi mtu aweza kujipasha joto mwenyewe? Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa, watu wawili wanaweza kumkabili adui na kumshinda. Kamba ya nyuzi tatu haikatiki kwa urahisi.