Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mhubiri 9:1-18

Mhubiri 9:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na kwa ajili ya hayo yote, nikatia moyo wangu katika kuyatafuta-tafuta haya; ya kuwa wenye haki, na wenye hekima, pamoja na matendo yao yote, wamo mkononi mwa Mungu; kwamba ni pendo au kwamba ni chuki, mwanadamu hajui; mambo yote yawapita. Mambo yote yawatukia wote sawasawa; kuna tukio moja kwake mwenye haki na kwake asiye haki; kwa mtu mwema na kwa mtu mwovu; kwa mtu aliye safi na kwa mtu asiye safi; kwake yeye atoaye kafara na kwake asiyetoa kafara; kama alivyo huyo mwema ndivyo alivyo mwenye dhambi; yeye aapaye na yeye aogopaye kiapo. Baa hilo ni katika mambo yote yanayofanyika chini ya jua, ya kuwa wote wanalo tukio moja; naam, zaidi ya hayo, mioyo ya wanadamu imejaa maovu, na wazimu umo mioyoni mwao wakati walipo hai, na baadaye huenda kwa wafu. Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa); kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua. Wewe enenda zako, ule chakula chako kwa furaha, unywe mvinyo yako kwa moyo wa kuchangamka; kwa kuwa Mungu amekwisha kuzikubali kazi zako. Mavazi yako na yawe meupe sikuzote; wala kichwa chako kisikose marhamu. Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua. Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe. Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote. Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamatwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu hunaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafula. Pia nimeona hekima chini ya jua, nayo ni kama hivi, tena kwangu mimi ilionekana kuwa ni neno kubwa. Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga. Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini. Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi. Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu. Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.

Shirikisha
Soma Mhubiri 9

Mhubiri 9:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Nilitafakari juu ya hayo yote, nikaona kwamba Mungu anaongoza matendo ya watu wenye hekima na waadilifu; ikiwa ni upendo au chuki, binadamu hajui. Kila kitu kwao ni bure kabisa, maana mwisho uleule huwapata waadilifu na waovu, wema na wabaya, walio safi na walio najisi, wenye kutoa sadaka na wasiotoa sadaka. Aliye mwema ni sawa tu na mwenye dhambi, na mwenye kuapa si tofauti na asiyeapa. Hili ni jambo baya zaidi kati ya yote yatukiayo hapa duniani, kwamba mwisho uleule huwapata wote. Tena, wakati wote wa maisha yao, wanadamu huwa wamejaa uovu na wazimu, na kisha hufa. Lakini anayeambatana na walio hai analo bado tumaini, afadhali mbwa hai kuliko simba mfu. Maana, walio hai hujua ya kwamba watakufa, lakini wafu hawajui chochote. Hawana tuzo tena; hata kumbukumbu lao limesahauliwa kabisa. Upendo wao, chuki zao na tamaa zao, vyote vimetoweka pamoja nao, na wala hawatashiriki chochote hapa duniani. Nenda ukale chakula chako kwa furaha, ukanywe na divai yako kwa moyo mchangamfu, maana Mungu amekwisha ikubali kazi yako. Vaa vizuri, jipake mafuta kichwani. Furahia maisha pamoja na mke wako umpendaye muda wote wa maisha yako ya bure ambayo Mungu amekujalia hapa duniani; maana hilo ndilo ulilopangiwa maishani, katika kazi zako hapa duniani. Kila unachotaka kufanya kifanye kwa nguvu zako zote, maana, hakuna kazi, wala wazo, wala maarifa, wala hekima huko kuzimu unakokwenda. Tena, nimeona kitu kimoja hapa duniani, kwamba wenye mbio hawafaulu katika riadha, wala wenye nguvu hawashindi vita; wenye busara hawapati chakula, wenye akili hawatajiriki, wala wenye ujuzi hawapandi vyeo; lakini wakati wa bahati huwapata wote pamoja. Mtu hajui saa yake itafika lini. Kama vile samaki wanavyonaswa katika wavu kwa bahati mbaya, na kama vile ndege wanavyonaswa katika mtego kwa ghafla, ndivyo wanadamu wanavyonaswa na balaa inapowaangukia bila ya kutazamia. Pia hapa duniani nimeona mfano wa hekima, na ulionekana kwangu kuwa wenye maana sana. Palikuwa na mji mmoja mdogo wenye wakazi wachache. Mfalme mmoja mwenye nguvu akafika, akauzingira na kujiandaa kuushambulia. Katika mji huo, alikuwapo maskini mmoja mwenye hekima, ambaye, kwa hekima yake aliuokoa mji huo. Lakini hakuna mtu aliyemkumbuka huyo maskini baadaye. Basi, mimi nasema, hekima ni bora kuliko nguvu, ingawa hekima ya maskini haithaminiwi, na maneno yake hayasikilizwi. Afadhali kusikiliza maneno matulivu ya mwenye hekima, kuliko kusikiliza kelele za mfalme katika kikao cha wapumbavu. Kuwa na hekima ni bora kuliko kutegemea silaha, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mazuri mengi.

Shirikisha
Soma Mhubiri 9

Mhubiri 9:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na kwa ajili ya hayo yote, nikatia moyo wangu katika kuyachunguza haya; ya kuwa wenye haki, na wenye hekima, pamoja na matendo yao yote, wamo mkononi mwa Mungu; iwe ni upendo au iwe ni chuki, mwanadamu hajui; mambo yote yawapita. Mambo yote yawatukia wote sawasawa; kuna tukio moja kwake mwenye haki na kwake asiye haki; kwa mtu mwema na kwa mtu mwovu; kwa mtu aliye safi na kwa mtu asiye safi; kwake yeye atoaye kafara na kwake asiyetoa kafara; kama alivyo huyo mwema ndivyo alivyo mwenye dhambi; yeye aapaye na yeye aogopaye kiapo. Baa hilo ni katika mambo yote yanayofanyika chini ya jua, ya kuwa wote wanalo tukio moja; naam, zaidi ya hayo, mioyo ya wanadamu imejaa maovu, na wazimu umo mioyoni mwao wakati walipo hai, na baadaye huenda kwa wafu. Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa; kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lolote, wala hawana tuzo tena; maana hata kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na chuki yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lolote lililofanyika chini ya jua. Wewe nenda zako, ule chakula chako kwa furaha, unywe mvinyo yako kwa moyo wa kuchangamka; kwa kuwa Mungu amekwisha kuzikubali kazi zako. Mavazi yako na yawe meupe sikuzote; wala kichwa chako kisikose manukato. Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana hiyo ni sehemu yako ya maisha; na katika kazi zako unazozifanya chini ya jua. Lolote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe. Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote. Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamatwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu hunaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafla. Pia nimeona mfano huu wa hekima chini ya jua, nao ni kama hivi, tena kwangu mimi ulionekana kuwa neno kubwa. Palikuwa na mji mdogo, uliokuwa na watu wachache ndani yake; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga. Basi, kulikuwemo na mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu yeyote aliyemkumbuka yule mtu maskini. Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; lakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi. Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu. Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.

Shirikisha
Soma Mhubiri 9

Mhubiri 9:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo niliyatafakari yote haya nikafikia uamuzi kwamba waadilifu na wenye hekima na yale wanayoyafanya yako mikononi mwa Mungu, lakini hakuna mtu ajuaye kama anangojewa na upendo au chuki. Wote wanayo hatima inayofanana, mwadilifu na mwovu, mwema na mbaya, aliye safi na aliye najisi, wale wanaotoa dhabihu na wale wasiotoa. Kama ilivyo kwa mtu mwema, ndivyo ilivyo kwa mtu mwenye dhambi; kama ilivyo kwa wale wanaoapa, ndivyo ilivyo kwa wale wasioapa. Huu ni ubaya ulio katika kila kitu kinachotendeka chini ya jua: Mwisho unaofanana huwapata wote. Zaidi ya hayo, mioyo ya watu, imejaa ubaya na kuna wazimu mioyoni mwao wangali hai, hatimaye huungana na waliokufa. Yeyote aliye miongoni mwa walio hai analo tumaini, hata mbwa hai ni bora kuliko simba aliyekufa! Kwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa, lakini wafu hawajui chochote, hawana tuzo zaidi, hata kumbukumbu yao imesahaulika. Upendo wao, chuki yao na wivu wao vimetoweka tangu kitambo, kamwe hawatakuwa tena na sehemu katika lolote linalotendeka chini ya jua. Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya. Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta. Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua. Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima. Nimeona kitu kingine tena chini ya jua: Si wenye mbio washindao mashindano au wenye nguvu washindao vita, wala si wenye hekima wapatao chakula au wenye akili nyingi wapatao mali, wala wenye elimu wapatao upendeleo, lakini fursa huwapata wote. Zaidi ya hayo, hakuna mwanadamu ajuaye wakati saa yake itakapokuja: Kama vile samaki wavuliwavyo katika wavu mkatili, au ndege wanaswavyo kwenye mtego, vivyo hivyo wanadamu hunaswa na nyakati mbaya zinazowaangukia bila kutazamia. Pia niliona chini ya jua mfano huu wa hekima ambao ulinivutia sana: Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzunguka akaweka jeshi kubwa dhidi yake. Katika mji huo kulikuwepo mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini. Kwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake. Maneno ya utulivu ya mwenye hekima husikiwa kuliko makelele ya mtawala wa wapumbavu. Hekima ni bora kuliko silaha za vita, lakini mwenye dhambi mmoja huharibu mema mengi.

Shirikisha
Soma Mhubiri 9