Esta 1:1-22
Esta 1:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Ahasuero, alipotawala ufalme wake ulikuwa mikoa 127, toka India hadi Kushi. Kiti chake cha enzi kilikuwa katika mji mkuu Susa. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wake, mfalme Ahasuero aliwaandalia karamu viongozi na watumishi wake wa serikali, wakuu wa majeshi ya Persia na Media, watu maarufu na wakuu wa mikoa. Basi, kwa muda wa miezi sita, Ahasuero akaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na fahari ya utawala wake. Muda huo ulipomalizika, mfalme aliwaandalia karamu watu wote wa mji mkuu wa Susa, wakubwa kwa wadogo. Karamu hiyo iliyochukua muda wa siku saba, ilifanyika uani, katika bustani ya ikulu. Mahali hapo palikuwa pamepambwa kwa mapazia ya pamba ya rangi nyeupe na vitambaa vya rangi ya buluu. Mapazia hayo yalikuwa yamefungiwa pete za fedha kwa kamba za kitani safi za zambarau, na kuninginizwa kwenye nguzo za marumaru. Makochi ya dhahabu na fedha yalikuwa yamewekwa kwenye sakafu iliyotengenezwa kwa vijiwe vya rangi, marumaru, lulumizi na mawe ya thamani. Watu walipewa vinywaji katika vikombe mbalimbali vya dhahabu, naye mfalme alikuwa mkarimu sana wa divai ya kifalme. Kila mtu alikunywa akashiba; mfalme alikuwa ametoa maagizo kwa watumishi wa ikulu wamhudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. Wakati huo huo, malkia Vashti naye aliwaandalia akina mama karamu ndani ya ikulu ya Ahasuero. Siku ya saba ya karamu hiyo, mfalme Ahasuero, akiwa amejaa furaha kutokana na divai aliyokuwa amekunywa, aliwaita matowashi saba waliomhudumia yeye binafsi: Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi. Aliwaamuru hao wamlete kwake malkia Vashti, akiwa amevaa taji yake ya kimalkia. Malkia huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, hivyo mfalme alitaka kuwaonesha wageni wake na viongozi uzuri wake. Lakini matowashi hao walipomweleza malkia amri ya mfalme, Vashti alikataa kutii. Jambo hilo lilimwudhi sana mfalme, akawa anawaka hasira moyoni. Ilikuwa desturi ya mfalme kupata mawaidha kutoka kwa wenye hekima, hivyo aliwaita wanasheria na mahakimu ili wamshauri la kufanya. Washauri wake wa kawaida walikuwa Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Maresi, Marsena na Memukani – viongozi saba wa Persia na Media waliokuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake. Aliwauliza hivi: “Je, kulingana na sheria, afanyiwe nini malkia Vashti? Maana, nimewatuma matowashi wangu kwake, lakini yeye amekataa kuitii amri yangu, mimi mfalme Ahasuero!” Hapo Memukani akamwambia mfalme na viongozi wake, “Licha ya kumkosea mfalme, malkia Vashti amewakosea viongozi na kila mtu katika mikoa ya mfalme Ahasuero! Tendo hili la malkia Vashti litajulikana na wanawake wote, nao watawadharau waume zao, wakisema: ‘Mfalme Ahasuero aliamuru malkia Vashti aje kwake, lakini yeye akakataa.’ Leo hii, mabibi wa Persia na Media ambao wamesikia alivyofanya malkia Vashti, watakuwa wanawaeleza viongozi wako; hivyo dharau na chuki vitajaa kila mahali. Basi, ukipenda, ewe mfalme, toa amri rasmi Vashti asije tena mbele yako. Amri hiyo na iandikwe katika sheria za Persia na Media, ili isiweze kubadilishwa. Kisha, cheo chake cha umalkia, apewe mwanamke mwingine anayestahili zaidi yake. Amri hiyo itakapotangazwa katika eneo lote la utawala wako, kila mwanamke atamheshimu mume wake, awe tajiri au maskini.” Wazo hilo lilimpendeza sana mfalme na viongozi wake, akatekeleza kama alivyopendekeza Memukani. Basi, akapeleka barua kwa kila mkoa kwa lugha na maandishi yanayoeleweka mkoani: Kwamba kila mwanamume awe bwana wa nyumba yake, na kuitangaza habari hii kwa lugha yake.
Esta 1:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika nyakati za Ahasuero; Ahasuero aliyetawala mikoa mia moja ishirini na saba, kutoka India mpaka Kushi; siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Susa, mji mkuu ngomeni; mwaka wa tatu wa kutawala kwake, ikawa aliwafanyia karamu wakuu na mawaziri wake; wakuu wa majeshi ya Uajemi na Umedi; watu maarufu na wakuu wa mikoa, wakihudhuria mbele zake. Akawaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, yaani siku mia moja na themanini. Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani mji mkuu, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika ukumbi wa bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawati, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu yenye nakshi ya vito vyekundu, marumaru, lulu za manjano na nyeusi na mawe ya thamani. Wakawanywesha kileo katika vyombo mbalimbali vya dhahabu, na divai tele ya kifalme, kufuatana na ukarimu wa ufalme; Walikunywa kama ilivyoamriwa, bila kushurutishwa; maana mfalme aliwaagiza watumishi wahudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake. Naye Vashti, malkia, akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Katika siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale Matowashi saba, wasimamizi wa nyumba saba waliohudumu mbele zake, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, akiwa amevaa taji la kifalme; ili kuwaonesha watu na wakuu uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, hakutii amri ya mfalme, alikataa kuja kama alivyoamriwa na mfalme kupitia kwa matowashi; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, waliojua sheria; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale wakuu saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi wa nyumba? Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na wakuu wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliozisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maofisa wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele. Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye. Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo. Basi neno hili likawapendeza mfalme na wakuu wake; naye mfalme akafanya kama alivyopendekeza Memukani. Kwa maana alipeleka nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake, ya kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake, na kuitangaza habari hii kwa lugha ya watu wake.
Esta 1:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Zamani za Ahasuero; naye huyu Ahasuero alimiliki toka Bara Hindi mpaka Kushi, juu ya majimbo mia na ishirini na saba; siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Shushani ngomeni; mwaka wa tatu wa kumiliki kwake, ikawa aliwafanyia karamu maakida wake wote na majumbe wake; wakuu wa Uajemi na Umedi, watu wenye cheo na maakida wa majimbo, wakihudhuria mbele zake. Akawaonyesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, maana siku mia na themanini. Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani ngomeni, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika behewa la bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawi, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu ya marumaru, mawe mekundu, na meupe, na ya manjano, na meusi. Wakawanywesha kileo katika vyombo vya dhahabu, na vile vyombo vilikuwa mbalimbali, na divai tele ya namna ya kifalme, sawasawa na ukarimu wa mfalme; kunywa kulikuwa kama ilivyoamriwa, bila sharti; maana ndivyo mfalme alivyowaagiza watumishi-wa-nyumbani, kila mtu afanye apendavyo. Tena Vashti, malkia, naye akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba? Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele. Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye. Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo. Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida; naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani. Kwa maana alipeleka nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake, ya kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake, na kuitangaza habari hii kwa lugha ya watu wake.
Esta 1:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ndilo lililotokea wakati wa utawala wa Mfalme Ahasuero, yule aliyetawala juu ya majimbo mia na ishirini na saba tangu Bara Hindi hadi Kushi. Wakati huo Mfalme Ahasuero alitawala katika kiti chake cha enzi katika ngome ya mji wa Shushani. Katika mwaka wa tatu wa utawala wake, alifanya karamu kwa ajili ya wakuu wake wote pamoja na maafisa. Akawaalika viongozi wa jeshi wa Uajemi na Umedi, wana wa wafalme na wakuu wa majimbo. Kwa siku zote 180 mfalme alionyesha utajiri mwingi wa ufalme wake, fahari na utukufu wa enzi yake. Siku hizo zilipopita, mfalme alifanya karamu kwa muda wa siku saba, katika bustani ya ndani katika jumba la kifalme, kwa ajili ya watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliokuwa katika ngome ya mji wa Shushani. Bustani ilikuwa na mapazia ya kitani nyeupe na buluu, yaliyofungiwa kamba za kitani nyeupe na kitambaa cha zambarau, kwenye pete za fedha juu ya nguzo za marmar. Kulikuwepo viti vya dhahabu na vya fedha vilivyokuwa vimewekwa kwenye ile sakafu iliyotengenezwa kwa mawe ya rangi, marmar, lulumizi na mawe mengine ya thamani. Vyombo vya dhahabu vilitumika kwa watu kunywea mvinyo, kila kimoja tofauti na kingine, naye mfalme akatoa mvinyo kwa wingi kwa kadiri ya ukarimu wake. Kwa amri ya mfalme kila mgeni aliruhusiwa kunywa alichotaka, kwa kuwa mfalme alitoa maagizo kwa watumishi wote wa kuhudumu mvinyo kumhudumia kila mtu kwa jinsi alivyotaka. Malkia Vashti pia akawafanyia wanawake karamu katika jumba la kifalme la Mfalme Ahasuero. Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani, Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi, kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aonyeshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri wa kupendeza. Lakini wakati watumishi walipotoa amri ya mfalme, Malkia Vashti alikataa kuja. Ndipo mfalme alighadhibika, na hasira yake ikawaka. Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati, nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake. Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.” Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’ Leo hii wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia juu ya tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwepo na mwisho wa dharau na magomvi. “Kwa hiyo, kama itampendeza mfalme, atoe amri ya kifalme na iandikwe katika sheria ya Uajemi na Umedi, ambayo haitabadilika, kwamba Vashti kamwe asije tena mbele ya Mfalme Ahasuero. Pia mfalme na atoe hiyo nafasi yake ya umalkia kwa mwanamke mwingine aliye bora kumliko yeye. Kisha mbiu hii ya mfalme itakapotangazwa katika himaya yake iliyo kubwa sana, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mdogo hadi mkubwa.” Mfalme na wakuu wake walipendezwa na shauri hili, hivyo basi mfalme akafanya kama Memukani alivyopendekeza. Alipeleka barua katika sehemu zote za ufalme wake, kwa kila jimbo kwa maandishi yake mwenyewe na kwa kila watu katika lugha yao wenyewe, akitangaza kwa msemo wa kila watu kwamba inampasa kila mwanaume kuwa mtawala wa nyumba yake mwenyewe.