Nembo ya Programu ya Biblia
Ikoni ya Utafutaji

Esta 2:5-8 - Linganisha Matoleo Yote

Esta 2:5-8 BHN (Biblia Habari Njema)

Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini. Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni. Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake. Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake.

Shirikisha
Esta 2 BHN

Esta 2:5-8 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Shushani ngomeni; jina lake Mordekai, bin Yairi, bin Shimei, bin Kishi, wa kabila ya Benyamini; ambaye kwamba amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alimchukua. Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye. Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake.

Shirikisha
Esta 2 SUV

Esta 2:5-8 SRUV (Swahili Revised Union Version)

Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Susa, mji mkuu; jina lake Mordekai, mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, wa kabila la Benyamini; ambaye alikuwa amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alimchukua. Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo nzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake. Basi amri ya mfalme na mbiu yake iliposikiwa, wasichana wengi wakakusanyika huko Susa, mji mkuu mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake.

Shirikisha
Esta 2 SRUV

Esta 2:5-8 NEN (Neno)

Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila la Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda. Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki. Agizo na amri ya mfalme ilipotangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa kwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake.

Shirikisha
Esta 2 NEN