Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 4:1-17

Esta 4:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mordekai alipojua yote yaliyotukia, alizirarua nguo zake, akavaa vazi la gunia, na kujitia majivu. Kisha, akapita katikati ya mji akilia kwa sauti ya uchungu. Alikwenda mpaka penye lango la ikulu ya mfalme, lakini hakuweza kuingia kwa sababu hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia ikulu akiwa amevaa vazi la gunia. Katika kila mkoa, mara tu amri ya mfalme ilipotangazwa, msiba mkubwa uliwakumba Wayahudi. Walifunga, wakalia na kuomboleza; na wengi wao walilala katika majivu wakiwa wamevaa magunia. Malkia Esta alipoarifiwa na matowashi na watumwa wa kike wake habari za Mordekai alihuzunika sana. Akampelekea Mordekai nguo za kuvaa badala ya vazi la gunia, lakini Mordekai akazikataa. Basi, akamwita Hathaki, mmoja wa matowashi wa mfalme aliyeteuliwa na mfalme amhudumie Esta, akamtuma kwa Mordekai kuuliza kisa na maana ya tukio hilo. Hathaki alimwendea Mordekai uwanjani, mbele ya lango la ikulu. Mordekai akamsimulia Hathaki yote yaliyokuwa yamempata, na kiasi kamili cha fedha ambayo Hamani alikuwa ameahidi kulipa katika hazina ya mfalme kama Wayahudi wote wangeangamizwa. Alimpa pia nakala moja ya tangazo lililokuwa limetolewa mjini Susa kuhusu kuangamizwa kwa Wayahudi, akamwomba amchukulie Esta, amweleze hali ilivyo, na kumwambia aende kumsihi mfalme na kumwomba awahurumie Wayahudi, watu wake Esta. Hathaki akaenda akamweleza Esta yote aliyosema Mordekai. Naye Esta akamwambia Hathaki arudi akamwambie Mordekai, “Watumishi wote wa mfalme na raia wa mikoa yote wanajua ya kwamba mtu yeyote yule akiingia katika ua wa ndani na kumwona mfalme bila kuitwa, huyo ni lazima auawe. Anayeweza kunusurika ni yule tu ambaye mfalme atamnyoshea fimbo yake ya dhahabu ili kumsalimisha. Kumbe mimi sijaitwa na mfalme, yapata mwezi mzima sasa.” Mordekai alipopata ujumbe wa Esta, mara alimpelekea onyo hili: “Usidhani kwamba kwa kuwa upo ikulu wewe u salama zaidi kuliko Myahudi mwingine yeyote yule. Ukikaa kimya wakati kama huu, msaada utawajia Wayahudi kutoka mahali pengine, nao wataokolewa; lakini wewe utakufa, na jamaa ya baba yako itaangamia. Ni nani ajuaye pengine umefanywa malkia kwa ajili ya wakati kama huu!” Esta alimpelekea Mordekai jibu hili: “Nenda ukawakusanye pamoja Wayahudi wote waliopo mjini Susa. Fungeni, msile wala msinywe kwa siku tatu, usiku na mchana, kwa ajili yangu. Na mimi na watumwa wa kike wangu tutafanya vivyo hivyo. Kisha, nitamwendea mfalme, ingawa ni kinyume cha sheria. Kama ni kuuawa, na niuawe.” Basi, Mordekai akaenda zake na kufanya kama Esta alivyomwambia.

Shirikisha
Soma Esta 4

Esta 4:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Mordekai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia na kujipaka majivu, akatoka hadi katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu. Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme akiwa amevaa magunia. Na katika kila mkoa, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu. Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; lakini yeye hakukubali. Kisha Esta akamwita Hathaki, towashi mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumue Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe. Pia akampa na nakala ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwoneshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake. Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai. Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema, Watumishi wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu yeyote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini. Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta. Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; lakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huu? Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Nenda ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Susa, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie. Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama vile Esta alivyomwagiza.

Shirikisha
Soma Esta 4

Esta 4:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu. Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia. Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu. Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; walakini yeye asikubali. Kisha Esta akamwita Hathaki, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumu Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini. Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme. Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliyoahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe. Pia akampa na nakili ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwonyeshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake. Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai. Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema, Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini. Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta. Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie. Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama vile Esta alivyomwagiza.

Shirikisha
Soma Esta 4

Esta 4:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini, akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu. Alikwenda akasimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa nguo za magunia. Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya nguo za magunia na majivu. Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya nguo za magunia, lakini Mordekai hakuzikubali. Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmojawapo wa matowashi wa mfalme ambaye alikuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta ni nini kilikuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini. Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme. Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi. Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonyesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake. Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai. Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai, “Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.” Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta, Mordekai alirudisha jibu hili: “Usifikiri kwamba kwa sababu uko katika nyumba ya mfalme wewe pekee katika Wayahudi wote utapona. Kwa kuwa kama utakaa kimya wakati huu, msaada na ukombozi kwa Wayahudi utatoka mahali pengine, lakini wewe na jamaa ya baba yako mtaangamia. Nani ajuaye kwamba hukuja kwenye nafasi ya mamlaka kwa ajili ya wakati kama huu?” Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai: “Nenda, kusanya pamoja Wayahudi wote walioko Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitakwenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.” Kwa hiyo Mordekai alikwenda zake na kutekeleza maagizo yote ya Esta.

Shirikisha
Soma Esta 4