Kutoka 14:10-18
Kutoka 14:10-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walipotazama na kumwona Farao akija na jeshi lake dhidi yao, walishikwa na hofu kubwa, wakamlilia Mwenyezi-Mungu. Wakamwambia Mose, “Je, hapakuwa na makaburi ya kutosha nchini Misri hata ukatuleta tufie huku jangwani? Mbona umetutendea haya, kwa tututoa katika nchi ya Misri? Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.” Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena. Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu. Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake. Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”
Kutoka 14:10-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli walipoangalia nyuma na kuona Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi wake.
Kutoka 14:10-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake.
Kutoka 14:10-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Farao alipokaribia, Waisraeli wakainua macho yao, wakawaona Wamisri wakija nyuma yao. Wakashikwa na hofu, wakamlilia BWANA. Wakamwambia Mose, “Je, ni kwamba hayakuwako makaburi huko Misri hata umetuleta tufe huku jangwani? Umetufanyia nini kututoa Misri? Hatukukuambia tulipokuwa huko Misri, tuache tuwatumikie Wamisri? Ingekuwa vyema zaidi kwetu kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani!” Mose akawajibu Waisraeli, “Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu BWANA atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu.” Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Kwa nini wewe unanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele. Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi BWANA nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”