Kutoka 15:22-27
Kutoka 15:22-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, Mose aliwaongoza Waisraeli kutoka bahari ya Shamu, wakaenda mpaka jangwa la Shuri. Walisafiri kwa muda wa siku tatu jangwani bila kuona maji yoyote. Walipofika mahali panapoitwa Mara, hawakuweza kuyanywa maji ya Mara kwa sababu yalikuwa machungu. Kwa sababu hiyo mahali hapo pakaitwa Mara. Basi, watu wote wakamlalamikia Mose wakisema, “Sasa tutakunywa nini?” Hapo Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamwonesha kipande cha mti, na Mose akakitumbukiza katika maji; maji hayo yakawa mazuri. Huko Mungu aliwapa Waisraeli amri na agizo, ili ajue uthabiti wao, akawaambia, “Ikiwa mtaisikiliza kwa makini sauti yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kutenda yaliyo sawa mbele yangu, na kuheshimu amri na maagizo yangu yote, basi, mimi sitawaletea yale magonjwa niliyowaletea Wamisri. Kwa sababu, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya nyinyi.” Kisha Waisraeli wakawasili huko Elimu ambako kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende sabini. Wakapiga kambi yao huko karibu na maji.
Kutoka 15:22-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji. Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini? Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawajaribu huko; akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yoyote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye. Wakafika Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapiga kambi hapo, karibu na maji.
Kutoka 15:22-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji. Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini? Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko; akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye. Wakafikilia Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapanga hapo, karibu na maji.
Kutoka 15:22-27 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kisha Musa akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara.) Kwa hiyo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, “Tunywe nini?” Ndipo Musa akamlilia Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akamwonesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu. Huko Mwenyezi Mungu akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. Mungu akasema, “Mkisikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuyafanya yaliyo mema machoni pake, na mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, niwaponyaye.” Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.