Kutoka 16:1-8
Kutoka 16:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Jumuiya yote ya Waisraeli iliondoka, ikafika jangwa la Sini kati ya Elimu na Sinai. Hii ilikuwa siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu walipoondoka nchini Misri. Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikawalalamikia Mose na Aroni huko jangwani, “Laiti Mwenyezi-Mungu angelituua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba. Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!” Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata. Lakini siku ya sita, wakati watakapoandaa chakula walichokusanya, kiasi hicho kitakuwa mara mbili ya chakula cha kila siku.” Basi, Mose na Aroni wakawaambia watu wote wa Israeli, “Jioni, mtatambua kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewatoa nchini Misri! Tena, kesho asubuhi, mtauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie?” Tena Mose akasema, “Jioni, Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama mle, na asubuhi atawapeni mikate mle mshibe, maana yeye ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie? Msitunungunikie sisi bali mnungunikieni Mwenyezi-Mungu.”
Kutoka 16:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikia jangwa la Sini, lililoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye husikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung'unikia? Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia yeye; na sisi tu nani? Manung'uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA.
Kutoka 16:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa BWANA katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa BWANA amewaleta kutoka nchi ya Misri; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa BWANA; kwa kuwa yeye asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia BWANA; na sisi tu nani, hata mkatunung’unikia? Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo BWANA atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa BWANA asikia manung’uniko yenu mliyomnung’unikia yeye; na sisi tu nani? Manung’uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya BWANA.
Kutoka 16:1-8 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani, jumuiya yote wakawanung’unikia Musa na Haruni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa Mwenyezi Mungu huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunung’unikie?” Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Mwenyezi Mungu wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manung’uniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnung’uniki dhidi yetu, bali dhidi ya Mwenyezi Mungu.”