Kutoka 2:11-15
Kutoka 2:11-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.
Kutoka 2:11-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku moja, baada ya Mose kukua, akaondoka kwenda walikokuwa watu wake, na akachunguza jinsi walivyokuwa wakifanya kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmojawapo wa watu wake. Mose akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha mchangani. Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?” Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Mose akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.” Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Mose, lakini Mose akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima.
Kutoka 2:11-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Mose alipokuwa mtu mzima, aliwaendea Waebrania wenzake ili kujionea taabu zao. Basi, akamwona Mmisri mmoja anampiga Mwebrania, mmoja wa ndugu zake Mose. Mose akatazama huku na huko, na alipoona kwamba hakuna mtu karibu, alimuua yule Mmisri na kumficha mchangani. Kesho yake, Mose alitoka tena, akaona Waebrania wawili wanapigana. Basi, akamwuliza yule aliyekosea, “Kwa nini unampiga mwenzako?” Naye akamjibu, “Nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi wetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Hivyo, Mose aliogopa na kufikiri, “Bila shaka jambo hilo limejulikana!” Naye Farao aliposikia juu ya tukio hilo akakusudia kumuua Mose. Lakini Mose alimkimbia Farao, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani. Siku moja, Mose alikuwa ameketi kando ya kisima cha maji.
Kutoka 2:11-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huku na huko, na alipoona ya kuwa hapakuwapo mtu, akampiga na kumwua Mmisri yule, akamfukia mchangani. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia kutoka kwa Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.