Kutoka 25:31-40
Kutoka 25:31-40 Biblia Habari Njema (BHN)
“Utatengeneza kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake na ufito wa hicho kinara vitakuwa kitu kimoja, kadhalika na vikombe vyake, matumba yake na maua yake, vyote vitafuliwa kwa kipande kimoja tu cha dhahabu. Matawi sita yatatokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine. Katika kila tawi kutakuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake. Na katika ufito kutakuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na vifundo vyake na maua yake. Mahali panapotokezea kila jozi ya matawi yale sita, chini yake patakuwa na kifundo kimojakimoja. Vifundo hivyo na matawi yake yatakuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kitafuliwa kwa dhahabu safi. Utatengeneza pia taa saba kwa ajili ya kinara hicho na kuziweka juu yake ili ziangaze kwa mbele. Tengeneza pia koleo zake na visahani vyake kwa dhahabu safi. Utatumia kilo thelathini na tano za dhahabu safi kutengeneza kinara hicho na vifaa vyake. Hakikisha kwamba umevitengeneza kwa mfano uliooneshwa kule mlimani.
Kutoka 25:31-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, kitako chake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho; nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili vikombe vitatu vilivyotengenezwa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara; na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake; na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara. Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi. Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake. Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi. Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote. Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, uliooneshwa mlimani.
Kutoka 25:31-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho; nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara; na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake; na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara. Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi. Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake. Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi. Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote. Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.
Kutoka 25:31-40 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Tengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi iliyofuliwa vizuri katika kitako chake na ufito wake; vikombe vyake vinavyofanana na ua, matovu yake na maua yake viwe kitu kimoja. Matawi sita yatatokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matatu upande mwingine. Vikombe vitatu vya mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua vitakuwa katika tawi moja, vikombe vitatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yanayotokeza kwenye kile kinara cha taa. Juu ya kinara chenyewe vitakuwa vikombe vinne vya mfano wa maua ya mlozi, yakiwa na matovu yake na maua yake. Tovu moja litakuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyotokeza kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla. Matovu na matawi yote yatakuwa kitu kimoja na kile kinara cha taa, yakifuliwa kwa dhahabu safi. “Kisha tengeneza taa zake saba na uziweke juu ya kinara hicho ili ziangaze mbele yake. Mikasi ya kusawazishia tambi, pamoja na masinia, zote zitakuwa za dhahabu safi. Utatumia talanta moja ya dhahabu safi kutengeneza hicho kinara na vifaa vyake vyote. Hakikisha kuwa umevitengeneza sawasawa na ule mfano uliooneshwa kule mlimani.