Kutoka 32:1-6
Kutoka 32:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu walipoona kuwa Mose amechelewa kurudi kutoka mlimani, walikusanyika mbele ya Aroni na kumwambia, “Haya! Tutengenezee miungu itakayotuongoza maana hatujui lililompata huyo Mose aliyetutoa nchini Misri.” Aroni akawajibu, “Chukueni vipuli vya dhahabu masikioni mwa wake zenu, wana wenu na binti zenu, mniletee.” Basi, watu wote wakatoa vipuli vyote vya dhahabu masikioni mwao, wakamletea Aroni. Naye akavichukua akaviyeyusha, akatengeneza ndama wa kusubu. Watu wakapaza sauti, “Ee Israeli, huyu ndiye mungu wetu aliyetutoa nchini Misri.” Kisha Aroni akamjengea huyo ndama madhabahu, halafu akatangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.” Kesho yake watu waliamka mapema wakatoa sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani. Watu wakaketi chini kula na kunywa; kisha wakasimama na kucheza.
Kutoka 32:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata. Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mniletee. Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni. Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa BWANA. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze.
Kutoka 32:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata. Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee. Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni. Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa BWANA. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze.
Kutoka 32:1-6 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Watu walipoona kuwa Musa amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimsonga Haruni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Musa aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui yaliyompata.” Haruni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu, na binti zenu wamevaa, mkaniletee.” Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Haruni. Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akasubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.” Haruni alipoona hili, akajenga madhabahu mbele ya yule ndama na kutangaza, “Kesho kutakuwa na sikukuu kwa Mwenyezi Mungu.” Kwa hiyo siku iliyofuata watu wakaamka asubuhi na mapema na kutoa sadaka za kuteketeza na sadaka za amani. Baadaye watu wakaketi kula na kunywa, nao wakasimama, wakajizamisha katika sherehe.