Kutoka 33:1-11
Kutoka 33:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Anza safari uondoke hapa, wewe na watu hao uliowatoa nchini Misri, mwende katika nchi niliyomwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo, nikisema, ‘Nitawapa wazawa wenu nchi hii’. Nitamtuma malaika awaongoze; nitawafukuza Wakaanani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Nendeni katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali. Lakini kwa sababu nyinyi ni wenye vichwa vigumu sitakwenda pamoja nanyi, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu walilia waliposikia habari hizi mbaya; wala hakuna aliyevaa mapambo yake. Walifanya hivyo kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu; nikienda pamoja nanyi kwa muda mfupi tu, nitawaangamiza. Hivyo vueni mapambo yenu ili nijue namna ya kuwatendea.’” Basi, Waisraeli waliyavua mapambo yao tangu walipoondoka mlimani Horebu. Mose alikuwa na desturi ya kulichukua lile hema na kulisimika nje ya kambi. Hema hilo alilipa jina, Hema la Mkutano. Mtu yeyote aliyetaka shauri kwa Mwenyezi-Mungu alikwenda kwenye hema la mkutano nje ya kambi. Kila mara Mose alipotoka kwenda kwenye hema hilo, kila mtu alisimama penye mlango wa hema lake na kumwangalia Mose mpaka alipoingia ndani ya hilo hema. Wakati Mose alipoingia ndani ya hilo hema, mnara wa wingu ulitua kwenye mlango wa hema, na Mwenyezi-Mungu akaongea naye. Watu wote walipouona ule mnara wa wingu umesimama mlangoni mwa hema, kila mmoja wao alisimama na kuabudu mlangoni mwa hema lake. Hivyo ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyokuwa akiongea na Mose uso kwa uso, kama mtu na rafiki yake. Kisha Mose alirudi tena kambini. Naye kijana Yoshua mwana wa Nuni ambaye alikuwa mtumishi wake hakuondoka hemani.
Kutoka 33:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yake. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni mapambo yenu ili nipate kujua nitakalowatenda. Basi wana wa Israeli wakavua mapambo yao, tangu mlima wa Horebu na mbele. Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya kambi na mbali hiyo kambi; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa BWANA, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya kambi. Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata kambini; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.
Kutoka 33:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda. Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele. Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa BWANA, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago. Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.
Kutoka 33:1-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’ Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ” Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu. Basi Musa alikuwa na desturi ya kuchukua hema na kuliweka wakfu nje ya kambi umbali kiasi, akaliita “Hema la Kukutania”. Kila aliyekuwa akiulizia shauri kwa Mwenyezi Mungu, angeenda hadi Hema la Kukutania, nje ya kambi. Wakati wowote Musa alipoenda kwenye Hema, watu wote waliinuka na kusimama kwenye maingilio ya mahema yao, wakimwangalia Musa hadi aingie kwenye Hema. Kila mara Musa alipoingia ndani ya Hema, nguzo ya wingu ingeshuka chini na kukaa kwenye ingilio, wakati Mwenyezi Mungu akizungumza na Musa. Kila mara watu walipoona hiyo nguzo ya wingu ikiwa imesimama kwenye ingilio la Hema, wote walisimama wakaabudu, kila mmoja kwenye ingilio la hema lake. Mwenyezi Mungu angezungumza na Musa uso kwa uso, kama vile mtu anavyozungumza na rafiki yake. Kisha Musa angerudi kambini, lakini msaidizi wake kijana Yoshua mwana wa Nuni hakuondoka kwenye Hema.