Kutoka 33:12-23
Kutoka 33:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama! Wewe waniambia, ‘Waongoze watu hawa,’ lakini hujanijulisha ni nani utakayemtuma anisaidie. Hata hivyo umesema kwamba unanijua kwa jina na pia kwamba nimepata fadhili mbele zako. Sasa basi, nakusihi, kama kweli nimepata fadhili mbele yako, nioneshe sasa njia zako, ili nipate kukujua na kupata fadhili mbele zako. Naomba ukumbuke pia kwamba taifa hili ni watu wako.” Mungu akasema, “Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe, na nitakupa faraja.” Mose akasema, “Kama wewe binafsi hutakwenda pamoja nami, basi, usituondoe mahali hapa. Maana nitajuaje kuwa nimepata fadhili mbele zako, mimi na watu wako kama usipokwenda pamoja nasi? Ukienda pamoja nasi itatufanya mimi na watu wako kuwa watu wa pekee miongoni mwa watu wote duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa kuwa umepata fadhili mbele yangu, nami nakujua kwa jina lako, jambo hilihili ulilolisema nitalifanya.” Mose akasema, “Nakusihi unioneshe utukufu wako.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nitapita mbele yako na kukuonesha wema wangu wote nikilitangaza jina langu, ‘Mwenyezi-Mungu’. Mimi nitamrehemu yule ninayependa kumrehemu, na kumhurumia yule ninayependa kumhurumia. Lakini hutaweza kuniona uso maana hakuna mwanadamu yeyote atakayeniona na kuishi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kuna mahali karibu nami ambapo utasimama juu ya mwamba; na utukufu wangu utakapokuwa unapita, nitakutia katika pango mwambani na kukufunika kwa mkono wangu, mpaka nitakapokuwa nimepita. Halafu nitauondoa mkono wangu nawe utaniona nyuma, lakini uso wangu hutauona.”
Kutoka 33:12-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Lakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unioneshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. Akasema, Nakusihi unioneshe utukufu wako. Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu. Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi. BWANA akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba; kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita; nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.
Kutoka 33:12-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako. Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu. Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi. BWANA akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba; kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita; nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.
Kutoka 33:12-23 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’ Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.” Mwenyezi Mungu akajibu, “Uso wangu utaenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.” Kisha Musa akamwambia, “Kama Uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa. Mtu yeyote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele zako, usipoenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?” Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nitakufanyia jambo lile uliloomba, kwa sababu ninapendezwa nawe, nami ninakujua kwa jina lako.” Kisha Musa akasema, “Basi nioneshe utukufu wako.” Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Mwenyezi Mungu, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.” Lakini Mungu akasema, “Hutaweza kuuona uso wangu, kwa kuwa hakuna mtu yeyote awezaye kuniona akaishi.” Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Kuna mahali karibu nami ambapo unaweza kusimama juu ya mwamba. Utukufu wangu unapopita, nitakuweka gengeni kwenye mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hadi nitakapokuwa nimepita. Kisha nitaondoa mkono wangu nawe utaona mgongo wangu; lakini kamwe uso wangu hautaonekana.”