Kutoka 35:1-19
Kutoka 35:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia BWANA ni haya, kwamba myafanye. Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa BWANA; mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa. Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato. Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema, Katwaeni kati yenu matoleo kwa BWANA; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba; na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na mbao za mshita; na mafuta kwa hiyo taa, na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri; na vito vya shohamu, na vito vya kutiwa kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani. Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo BWANA ameyaagiza; yaani, hiyo maskani na hema yake, na kifuniko chake, na vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na viguzo vyake, na matako yake; hilo sanduku, na miti yake, na hicho kiti cha rehema, na lile pazia la sitara; na hiyo meza, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hiyo mikate ya wonyesho; na hicho kinara cha taa kwa mwanga, na vyombo vyake, na taa zake, na hayo mafuta kwa nuru; na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, na miti yake, na hayo mafuta ya kupaka, na huo uvumba mzuri, na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hilo birika na tako lake; na hizo kuta za nguo za ua, na viguzo vyake, na matako yake, na pazia la lango la ua; na vile vigingi vya maskani, na vigingi vya ua, na kamba zake na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
Kutoka 35:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose alikusanya jumuiya yote ya Waisraeli, akawaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo Mwenyezi-Mungu amewaamuru muyafanye: Kwa siku sita mtafanya kazi zenu; lakini siku ya saba ni Sabato siku ya mapumziko ambayo ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima auawe. Msiwashe hata moto katika makao yenu siku ya Sabato.” Mose aliiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo jambo ambalo Mwenyezi-Mungu amewaamuru mlifanye: Mtatoa katika mali zenu mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu. Kila mtu mwenye moyo mwema atamletea Mwenyezi-Mungu mchango: Dhahabu, fedha, shaba; sufu ya buluu, ya zambarau na nyekundu; kitani safi iliyosokotwa; manyoya ya mbuzi; ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za mbuzi; mbao za mjohoro, mafuta kwa ajili ya taa, viungo kwa ajili ya mafuta ya kupaka na kwa ajili ya ubani wenye harufu nzuri; vito vya sardoniki na vito vingine kwa ajili ya mapambo ya kizibao na kifuko cha kifuani. “Kila mtu mwenye ujuzi wa kazi fulani miongoni mwenu atakuja kufanya vitu vyote alivyoamuru Mwenyezi-Mungu: Kutengeneza hema takatifu, kifuniko chake na pazia lake, kulabu zake, pau zake, vikalio vyake; sanduku la agano pamoja na mipiko yake, kiti cha rehema, pazia la mahali patakatifu sana; meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; vinara vya taa pamoja na vyombo vyake vyote, taa zake na mafuta yake; madhabahu ya ubani na mipiko yake, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri, pazia la mlango wa hema takatifu; madhabahu ya sadaka za kuteketezwa pamoja na wavu wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, birika na tako lake; vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake, pazia la mlango wa ua; vigingi vya hema takatifu na vya ua pamoja na kamba zake; mavazi yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na ya wanawe, kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani.”
Kutoka 35:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia BWANA ni haya, kwamba myafanye. Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa BWANA; mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo atauawa. Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato. Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema, Katwaeni kati yenu matoleo kwa BWANA; mtu yeyote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba; na nyuzi za rangi ya buluu, zambarau, nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi; na ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za pomboo na mbao za mshita; na mafuta kwa hiyo taa, na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri; na vito vya shohamu, vito vya kutiwa kwa hiyo naivera na kwa hicho kifuko cha kifuani. Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo BWANA ameyaagiza; yaani, hiyo maskani na hema yake, kifuniko chake, vifungo vyake, mbao zake, mataruma yake, viguzo vyake na vitako vyake; hilo sanduku, miti yake, hicho kiti cha rehema na lile pazia la sitara; na hiyo meza, miti yake, vyombo vyake vyote na hiyo mikate ya wonyesho; na hicho kinara cha taa kwa mwanga, vyombo vyake, taa zake na hayo mafuta kwa nuru; na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, miti yake, hayo mafuta ya kupaka, huo uvumba mzuri na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, miti yake, vyombo vyake vyote hilo birika na kitako chake; na hizo kuta za nguo za ua, viguzo vyake, vitako vyake na pazia la lango la ua; na vile vigingi vya maskani, vigingi vya ua na kamba zake na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
Kutoka 35:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mose akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo BWANA amewaamuru ninyi mfanye: Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya kupumzika kwa BWANA. Yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe. Msiwashe moto mahali popote katika makazi yenu siku ya Sabato.” Mose akaiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo BWANA aliloamuru: Toeni sadaka kwa BWANA kutoka mali mliyo nayo. Kila mmoja aliye na moyo wa kupenda atamletea BWANA sadaka ya dhahabu, fedha na shaba; nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi; singa za mbuzi; ngozi za kondoo dume zilizopakwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo; mbao za mshita; mafuta ya zeituni kwa ajili ya taa; vikolezi kwa ajili ya mafuta ya upako, pamoja na uvumba wa harufu nzuri; vito vya shohamu, na vito vingine vya thamani vya kuweka kwenye kisibau na kile kifuko cha kifuani. “Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kitu BWANA alichoamuru: Maskani pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako; Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia; meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonyesho; kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga; madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri; pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya maskani; madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote; sinia la shaba pamoja na tako lake; pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, pazia la ingilio la kwenye ua; vigingi vya hema kwa ajili ya maskani pamoja na ua na kamba zake; mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.”