Kutoka 35:30-35
Kutoka 35:30-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, BWANA amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; naye amemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina; na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, na fedha, na shaba, na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za werevu kila aina. Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.
Kutoka 35:30-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose aliwaambia Waisraeli; “Tazameni! Mwenyezi-Mungu amemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda. Amemjaza roho yake, amempa ujuzi, akili, maarifa na ufundi, abuni michoro ya sanaa na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba; achonge mawe ya kupambia na mbao kwa ajili ya kazi nyingine zote za kifundi. Pia amemwongoza yeye na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani wawafundishe wengine. Amewapa ujuzi wa kufanya kila kazi ya ufundi au ifanywayo na watu wa sanaa au mafundi wa kutarizi kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kwa kutumia ufundi wowote wa msanii.
Kutoka 35:30-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, BWANA amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda; naye amemjaza Roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina; na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, fedha na shaba, na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za ufundi wa kila aina. Naye amemtilia moyoni mwake uwezo ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani. Amewajaza watu hao ujuzi, ili watumike katika kazi za kila aina, mawe, na kazi ya fundi mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri, ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yoyote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.
Kutoka 35:30-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Mose akawaambia Waisraeli, “Tazameni, BWANA amemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, naye amemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, na uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi wa kupendeza. Tena amempa yeye pamoja na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, uwezo wa kufundisha wengine. Amewajaza ustadi wa kufanya kazi za aina zote zifanywazo na mafundi, na wenye kubuni michoro, pia na watarizi kwa rangi za buluu, zambarau, nyekundu na kitani safi, na wafumaji: wote wakiwa mafundi na wabunifu hodari.