Kutoka 4:18-31
Kutoka 4:18-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose alirudi kwa Yethro, baba mkwe wake, akamwambia, “Tafadhali niruhusu nirudi Misri kwa ndugu zangu, nikaone kama bado wako hai.” Yethro akamwambia, “Nenda kwa amani.” Mose akiwa bado nchini Midiani, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi Misri kwa sababu wale wote waliotaka kukuua wamekwisha kufa.” Basi, Mose akamchukua mkewe na watoto wake, akawapandisha juu ya punda, akaanza safari ya kurudi Misri. Mkononi mwake alichukua ile fimbo aliyoamriwa na Mungu aichukue. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utakapofika Misri, hakikisha kwamba umetenda mbele ya Farao miujiza yote niliyokupa uwezo kuifanya. Lakini mimi nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hatawaachia Waisraeli waondoke. Nawe utamwambia Farao kuwa Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Israeli ni mzaliwa wangu wa kwanza wa kiume! Nami nakuambia: Mwache mwanangu aondoke, ili anitumikie! Kama ukikataa kumwachia aondoke, tazama nitamuua mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.’” Akiwa bado njiani kurudi Misri, Mose alikuwa mahali pa kulala wageni; basi, Mungu alikutana naye na kutaka kumuua. Hapo Zipora akakimbia haraka, akachukua jiwe kali, akalikata govi la mwanawe na kumgusa nalo Mose miguuni akisema, “Wewe ni bwana harusi wa damu”. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwacha Mose. Zipora alikuwa amesema, “Bwana harusi wa damu,” kwa sababu ya kutahiri. Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukakutane na Mose.” Basi, Aroni akaenda, akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu. Naye Mose akamwambia Aroni maneno yote aliyoambiwa na Mwenyezi-Mungu ayaseme, na miujiza yote aliyoagizwa atende. Kisha Mose na Aroni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli. Aroni akawaambia maneno yote Mwenyezi-Mungu aliyokuwa amemwagiza Mose, na kuifanya ile miujiza mbele ya watu wote. Watu wakaamini. Na waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu amewajia kuwasaidia Waisraeli, na kwamba ameyaona mateso yao, wote wakainamisha vichwa vyao na kumwabudu.
Kutoka 4:18-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani. BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, rudi Misri; kwa kuwa wale watu wote walioutaka uhai wako wamekwisha kufa. Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako. Ndipo walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye, akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu lenye makali na kulikata govi ya zunga la mwanawe, na kulibwaga miguuni pa Musa akasema. Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri. BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu. Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza. Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli. Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu. Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainamisha vichwa vyao wakasujudu.
Kutoka 4:18-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani. BWANA akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, karudi Misri; kwa kuwa wale watu wote waliokutaka uhai wako wamekwisha kufa. Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako. Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri. BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu. Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza. Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli. Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu. Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu.
Kutoka 4:18-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Mose akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.” Yethro akamwambia, “Nenda, nami nakutakia mema.” Basi BWANA alikuwa amemwambia Mose huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.” Basi Mose akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. BWANA akamwambia Mose, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili kwamba asiwaruhusu watu waende. Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza, nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu kwenda, basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ” Mose alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, BWANA akakutana naye, akataka kumuua. Lakini Sipora akachukua jiwe gumu, akakata govi la mwanawe na kugusa nalo miguu ya Mose. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.” Sipora alipomwita Mose, “Bwana arusi wa damu,” alikuwa anamaanisha ile tohara. Baada ya hayo BWANA akamwacha. BWANA akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukamlaki Mose.” Basi akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu. Kisha Mose akamwambia Aroni kila kitu BWANA alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya. Mose na Aroni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli, naye Aroni akawaambia kila kitu BWANA alichokuwa amemwambia Mose. Pia akafanya ishara mbele ya watu, nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa BWANA anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.