Kutoka 6:1-8
Kutoka 6:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Sasa utaona jinsi nitakavyomtenda Farao; maana kwa nguvu atalazimika kuwaacha watu wangu watoke. Naam, kwa nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.” Mungu akamwambia Mose, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nilimtokea Abrahamu, Isaka na Yakobo nikijulikana kama Mungu Mwenye Nguvu, ingawa kwa jina langu, Mwenyezi-Mungu, sikuwajulisha. Tena nilifanya agano nao kwamba nitawapa nchi ya Kanaani ambako waliishi kama wageni. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha Waisraeli ambao wamelazimishwa kufanya kazi za kitumwa na Wamisri, nikalikumbuka agano langu. Kwa hiyo, waambie Waisraeli hivi, ‘Mimi ni Mwenyezi-Mungu! Mimi nitawatoa katika nira mlizowekewa na Wamisri. Nitawaokoeni utumwani mwenu. Nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuwaadhibu vikali Wamisri na kuwakomboa nyinyi. Nitawafanyeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nyinyi mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nira za Wamisri. Nami nitawapeleka katika nchi ile niliyoapa kumpa Abrahamu, Isaka na Yakobo. Nitawapeni nchi hiyo iwe yenu. Mimi ni Mwenyezi-Mungu.’”
Kutoka 6:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni BWANA; nami nilimtokea Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya waliyokaa kama wageni. Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni BWANA nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya ukandamizaji wa Wamisri, nami nitawaokoa kutoka utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwakomboaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo niliinua mkono wangu, niwape Abrahamu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA.
Kutoka 6:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA.
Kutoka 6:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akamwambia Mose, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.” Pia Mungu akamwambia Mose, “Mimi ndimi BWANA. Nilimtokea Abrahamu, Isaki na Yakobo kama Mungu Mwenyezi, ingawa sikuwajulisha Jina langu, Yehova, Mimi mwenyewe sikujitambulisha kwao. Pia niliweka Agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka Agano langu. “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi BWANA, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. Nitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi BWANA.’ ”