Kutoka 8:16-19
Kutoka 8:16-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yatageuka kuwa viroboto kote nchini Misri.” Mose na Aroni wakafanya hivyo. Aroni alinyosha fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yakageuka kuwa viroboto na kuwaparamia watu na wanyama. Mavumbi yote nchini kote Misri yakageuka kuwa viroboto. Wachawi wa Misri, kwa uchawi wao, wakajaribu kuyageuza mavumbi yawe viroboto, lakini hawakufaulu. Viroboto hao wakaenea juu ya watu na wanyama. Wale wachawi wakamwambia Farao, “Hii ni kazi ya mkono wa Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukaendelea kuwa mgumu; wala hakuwasikiliza Mose na Aroni. Ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.
Kutoka 8:16-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. Nao wakafanya hivyo; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri. Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni kidole cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.
Kutoka 8:16-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri. Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.
Kutoka 8:16-19 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.” Wakafanya hivyo, Haruni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto. Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama. Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.