Kutoka 8:20-32
Kutoka 8:20-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho amka asubuhi mapema umwendee Farao wakati anapokwenda mtoni umwambie, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie. Kama ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitakuletea makundi ya nzi, wewe, maofisa wako na watu wako wote. Wataingia kwenye nyumba zenu na nyumba zote za Wamisri zitajaa makundi ya nzi, kadhalika na ardhi yote ya Misri. Lakini siku hiyo sehemu ya Gosheni wanakoishi watu wangu nitaikinga: Humo nzi hao hawatakuwamo. Hapo ndipo utakapotambua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu natenda mambo nchini mwako. Nitawakinga watu wangu na mambo yatakayowapata watu wako. Mambo hayo yatafanyika kesho.’” Mwenyezi-Mungu akafanya kama alivyosema: Makundi makubwa ya nzi yakaivamia nyumba ya Farao, nyumba za maofisa wake na nchi nzima ya Misri. Nchi nzima ya Misri ikaharibiwa na nzi hao. Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni, akasema, “Mnaweza kwenda kumtambikia Mungu wenu, lakini iwe humuhumu nchini Misri.” Lakini Mose akamjibu, “La! Haifai kufanya hivyo, maana tambiko tutakazomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, zitawachukiza Wamisri. Je, Wamisri wakituona tukitoa tambiko ambazo ni chukizo kwao, si watatupiga mawe? Ni lazima tusafiri mwendo wa siku tatu jangwani tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama atakavyotuamuru.” Basi, Farao akasema, “Nitawaacha mwende zenu kumtambikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, jangwani. Walakini msiende mbali mno. Niombeeni na mimi.” Mose akamjibu, “Mara tu nitakapokuacha, nitamwomba Mwenyezi-Mungu makundi haya ya nzi yatoweke kwako wewe Farao, maofisa wako na watu wako, kesho. Lakini wewe usitudanganye tena kwa kukataa kuwaacha watu kwenda kumtambikia Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mose akaondoka nyumbani kwa Farao, akamwomba Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba, wale nzi wakatoweka kutoka kwa Farao, maofisa wake na watu wake, wala hakusalia hata mmoja. Lakini hata safari hii Farao alikuwa mkaidi, wala hakuwaruhusu Waisraeli kuondoka.
Kutoka 8:20-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta inzi wengi sana juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na inzi wengi sana, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao inzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia. Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho. BWANA akafanya; wakaja inzi wengi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa na wale inzi. Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii. Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka BWANA, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe? La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu BWANA, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza. Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu BWANA, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni. Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba BWANA ili hao inzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia BWANA dhabihu. Musa akatoka kwa Farao, akamwomba BWANA. BWANA akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale inzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja. Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.
Kutoka 8:20-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia. Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho. BWANA akafanya; wakaja wingi wa mainzi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa kwa ajili ya wale mainzi. Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii. Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka BWANA, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe? La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu BWANA, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza. Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu BWANA, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni. Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba BWANA ili hao mainzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia BWANA dhabihu. Musa akatoka kwa Farao, akamwomba BWANA. BWANA akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale mainzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja. Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.
Kutoka 8:20-32 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo BWANA asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri. “ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, BWANA, niko katika nchi hii. Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ” Naye BWANA akafanya hivyo. Makundi makubwa ya mainzi yalimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na mainzi. Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.” Lakini Mose akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea BWANA Mungu wetu zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Kama tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe? Ni lazima twende mwendo wa siku tatu mpaka tufike jangwani ili tumtolee BWANA Mungu wetu dhabihu, kama alivyotuagiza.” Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea BWANA Mungu wenu dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.” Mose akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba BWANA na kesho mainzi yataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake. Hakikisha tu kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea BWANA dhabihu.” Ndipo Mose akamwacha Farao na kumwomba BWANA, naye BWANA akafanya lile Mose alilomwomba. Mainzi yakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia. Lakini wakati huu pia Farao akaushupaza moyo wake, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.