Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 1:1-14

Ezekieli 1:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo siku ya tano ya mwezi wa nne, mwaka wa thelathini, nilikuwa Babuloni kwenye mto Kebari miongoni mwa wale watu waliopelekwa uhamishoni. Basi, mbingu zilifunguka, nikaona maono ya Mungu. Katika siku hiyo ya tano ya mwezi (ulikuwa mwaka wa tano baada ya mfalme Yehoyakini kupelekwa uhamishoni Babuloni), Mwenyezi-Mungu aliongea nami kuhani Ezekieli mwana wa Buzi, nilipokuwa Kaldayo karibu na mto Kebari, naye Mwenyezi-Mungu akaniwekea mkono wake. Nilipotazama niliona upepo wa dhoruba unavuma kutoka kaskazini: Kulikuwa na wingu kubwa lililozungukwa na mngao, na moto ulichomoza humo mfululizo na katikati ya huo moto kulikuwa na kitu kinametameta kama shaba. Kutoka humo nilibainisha viumbe hai wanne, ambao walionekana hivi: Walikuwa na umbo la binadamu. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyoka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Walikuwa na mikono ya binadamu chini ya mabawa yao katika pande zao nne. Ncha za mabawa yao ziligusana kila bawa na bawa lingine. Waliposogea, upande wowote ule, walikwenda mbele moja kwa moja bila kugeuza miili yao. Kuhusu nyuso zao nne kila mmoja wao alikuwa na uso wa binadamu upande wa mbele, uso wa simba upande wa kulia, uso wa ng'ombe upande wa kushoto, na uso wa tai upande wa nyuma. Mabawa mawili ya kila mmoja yalikuwa yamekunjuliwa juu na kugusana na kwa mabawa yale mengine mawili walifunika miili yao. Popote roho ilipotaka kwenda, walikwenda; kila mmoja wao alikwenda mbele moja kwa moja bila kuugeuza mwili wake. Katikati ya hao viumbe hai kulikuwa na kitu kilichoonekana kama makaa yanayowaka moto, kama miali ya moto iliyomulika huku na huko kati ya hao viumbe. Moto huo ulikuwa mwangavu na umeme ulichomoza humo. Viumbe hao pia walikwenda huku na huko kama pigo la umeme.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1

Ezekieli 1:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu. Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne. Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana. Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi; mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kulia; na hao wanne walikuwa na uso wa ng'ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda. Kwa habari za kuonekana kwao wale viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya wale viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme. Na wale viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1

Ezekieli 1:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu. Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa BWANA ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne. Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana. Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi; mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda. Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme. Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1

Ezekieli 1:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, wakati nilipokuwa miongoni mwa hao waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu. Katika siku ya tano ya mwezi, ilikuwa mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehayakini, neno la BWANA lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa BWANA ulikuwa juu yake. Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini, wingu kubwa sana pamoja likiwa na umeme wa radi likiwa limezungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama rangi ya manjano ya chuma kinapokuwa ndani ya moto. Katika ule moto kulikuwa na kitu kinachofanana na viumbe vinne vyenye uhai. Katika kuonekana kwake vilikuwa na umbo mfano wa mwanadamu, lakini kila kimoja kilikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka, nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja, hawakugeuka walipokuwa wanatembea. Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa wale wanne alikuwa na uso wa mwanadamu na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, upande wa kushoto alikuwa na uso wa ngʼombe pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Mabawa yao yalikunjuliwa kuelekea juu, kila mmoja alikuwa na mabawa mawili ambayo kila moja liligusa bawa la mwenzake kila upande na mabawa mengine mawili yakifunika mwili wake. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipotaka kwenda, ndipo walipokwenda pasipo kugeuka. Kuonekana kwa vile viumbe hai katikati kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya vile viumbe, ulikuwa na mwangaza mkali na katikati ya ule moto kulitoka kimulimuli kama umeme wa radi. Vile viumbe vilipiga mbio kwenda na kurudi, kama vimulimuli vya umeme wa radi.

Shirikisha
Soma Ezekieli 1