Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:1-17

Ezekieli 20:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwaka wa saba tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa tano, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja kumwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, wakaketi mbele yangu. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Wewe mtu, sema na hao wazee wa Israeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Je, mmekuja kuniuliza shauri? Hakika, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema kuwa sitakubali kuulizwa kitu na nyinyi. “Wewe mtu, je, uko tayari kuwahukumu watu hawa? Basi, wahukumu. Wajulishe waliyofanya wazee wao. Waambie kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nilipowachagua Waisraeli niliwaapia wazawa wa Yakobo. Nilijidhihirisha kwao nchini Misri, nikawaapia nikisema: Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Siku hiyo niliwaapia kwamba nitawatoa nchini Misri na kuwaongoza mpaka kwenye nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Niliwaambia: ‘Tupilieni mbali machukizo yote mnayoyapenda; msijitie unajisi kwa sanamu za miungu ya Misri, kwa maana mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.’ Lakini waliniasi, hawakutaka kunisikiliza. Hakuna hata mmoja wao aliyetupilia mbali machukizo yale waliyoyapenda, wala hawakuachana na sanamu za miungu ya Misri. Basi, nikafikiri kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao wakiwa kulekule nchini Misri. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa heshima ya jina langu ili lisidharauliwe kati ya watu wa mataifa wanaoishi nao, hao walioona nikijijulisha kwa Waisraeli wakati wa kuwatoa katika nchi ya Misri. “Basi, mimi niliwatoa nchini Misri, nikawapeleka jangwani. Niliwapa kanuni zangu na kuwafundisha amri zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Niliwapa pia Sabato zangu ziwe ishara kati yangu na wao, wapate kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa. Lakini Waisraeli waliniasi huko jangwani; hawakuzifuata kanuni zangu, bali walizikataa sheria zangu ambazo mtu akizifuata huishi. Sabato zangu walizikufuru daima, nami nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuwaangamiza hukohuko jangwani. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa ambao walishuhudia jinsi nilivyowatoa Waisraeli nchini Misri. Hata hivyo, niliwaapia kulekule jangwani kwamba sitawaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote. Nilifanya hivyo kwa sababu walizikataa kanuni zangu na kuzikufuru Sabato zangu; kwani walipania kwa moyo sanamu za miungu yao. Lakini nilisalimisha maisha yao, sikuwaangamiza kule jangwani.

Ezekieli 20:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao; uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni BWANA, Mungu wenu; katika siku ile niliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, itiririkayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu. Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri. Lakini nilitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nilijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani. Nikawapa amri zangu, na kuwaonesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda. Tena niliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye. Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize. Lakini nilitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao niliwatoa mbele ya macho yao. Tena niliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, itiririkayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao. Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.

Ezekieli 20:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi. Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao; uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni BWANA, Mungu wenu; katika siku ile naliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni BWANA, Mungu wenu. Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri. Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nalijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani. Nikawapa amri zangu, na kuwaonyesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda. Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye. Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize. Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao naliwatoa mbele ya macho yao. Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote; kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao. Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.

Ezekieli 20:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa saba, mwezi wa tano siku ya kumi, baadhi ya wazee wa Israeli wakaja ili kutaka ushauri kwa BWANA, wakaketi mbele yangu. Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa nini mmekuja? Je, ni kutaka ushauri kwangu? Hakika kama niishivyo, sitawaruhusu mtake ushauri toka kwangu, asema BWANA Mwenyezi.’ “Je, utawahukumu? Je, mwanadamu, utawahukumu? Basi uwakabili kwa ajili ya machukizo ya baba zao na uwaambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Siku ile nilipochagua Israeli, niliwaapia wazao wa nyumba ya Yakobo kwa mkono ulioinuliwa nami nikajidhihirisha kwao huko Misri. Kwa mkono ulioinuliwa niliwaambia, “Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” Siku ile niliwaapia wao kwamba nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta katika nchi niliyowachagulia, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi nzuri kupita zote. Nami nikawaambia, “Kila mmoja wenu aondolee mbali sanamu za chukizo ambazo mmekazia macho, nanyi msijitie unajisi kwa sanamu za Misri. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” “ ‘Lakini waliniasi na hawakunisikiliza, hawakuondolea mbali sanamu za machukizo ambazo walikuwa wamezikazia macho, wala kuondolea mbali sanamu za Misri. Ndipo nikasema, nitawamwagia ghadhabu yangu na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko Misri. Lakini kwa ajili ya Jina langu nilifanya kile ambacho kingelifanya lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa waliyoishi miongoni mwao na ambao machoni pao nilikuwa nimejifunua kwa Waisraeli kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Kwa hiyo nikawaongoza watoke Misri na kuwaleta jangwani. Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi BWANA niliwafanya kuwa watakatifu. “ ‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani. Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba nisingewaingiza katika nchi niliyokuwa nimewapa, yaani, nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi nzuri kuliko zote, kwa sababu walikataa sheria zangu na hawakufuata amri zangu na wakazinajisi Sabato zangu. Kwa kuwa mioyo yao iliandama sanamu zao. Lakini niliwahurumia wala sikuwaangamiza wala hakuwafuta kabisa jangwani.