Ezekieli 21:1-17
Ezekieli 21:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ugeukie mji wa Yerusalemu, uhubiri dhidi ya sehemu zake za ibada, na kutoa unabii juu ya nchi ya Israeli. Waambie Waisraeli kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe naja kupambana nanyi. Nitauchomoa upanga wangu alani mwake na kuwaua watu wema na wabaya. Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu. Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani. “Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao. Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Upanga! Naam, upanga umenolewa, nao umengarishwa pia. Umenolewa ili ufanye mauaji, umengarishwa umetamete kama umeme! Umenolewa na kungarishwa uwekwe mkononi mwa mwuaji. Wewe mtu, lia na kuomboleza upanga huo umenyoshwa dhidi ya watu wangu, dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wataangamizwa kwa upanga pamoja na watu wangu. Jipige kifua kwa huzuni. Hilo litakuwa jaribio gumu sana. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe mtu, tabiri! Piga makofi, upanga na ufanye kazi yake, mara mbili, mara tatu. Huo ni upanga wa mauaji nao unawazunguka. Kwa hiyo wamekufa moyo na wengi wanaanguka. Ncha ya upanga nimeiweka katika malango yao yote. Umefanywa ungae kama umeme, umengarishwa kwa ajili ya mauaji. Ewe upanga, shambulia kulia, shambulia kushoto; elekeza ncha yako pande zote. Nami nitapiga makofi, nitatosheleza ghadhabu yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 21:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli; uiambie nchi ya Israeli, BWANA asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya. Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mwovu, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hadi kaskazini, na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena. Piga kite, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika moyo na uchungu mwingi mbele ya macho yao. Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unapiga kite? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatageuka kuwa kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa, umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti. Nao umetolewa ili ung'arishwe upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye. Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani. Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU. Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote. Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje. Jiweke tayari, nenda upande wa kulia; jipange, nenda upande wa kushoto; mahali popote utakapouelekeza uso wako. Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili.
Ezekieli 21:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako kuelekea Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli; uiambie nchi ya Israeli, BWANA asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya. Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hata kaskazini, na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena. Ugua, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika kwake viuno vyako, na kwa uchungu, utaugua mbele ya macho yao. Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unaugua? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatalegea kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa, umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti. Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye. Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani. Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU. Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote. Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje. Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako. Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili.
Ezekieli 21:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli uiambie: ‘Hili ndilo BWANA asemalo: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu. Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utakuwa wazi dhidi ya kila mmoja kuanzia kusini mpaka kaskazini. Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi BWANA nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’ “Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi. Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatokea, asema BWANA Mwenyezi.” Neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: “ ‘Upanga, upanga, ulionolewa na kusuguliwa: umenolewa kwa ajili ya mauaji, umesuguliwa ili ungʼae kama umeme wa radi! “ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unaidharau kila fimbo ya namna hiyo. “ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa, ili upate kushikwa mkononi, umenolewa na kusuguliwa, umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji. Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu, kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu; u dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa wauawe kwa upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo pigapiga kifua chako. “ ‘Kwa maana upanga huu umejaribiwa na kuhakikishwa, itakuwaje basi fimbo ya ufalme ya Yuda inayoudharau kama haitakuwepo tena, bali itakuwa imeondolewa kabisa? asema BWANA Mwenyezi.’ “Hivyo basi, mwanadamu, tabiri na ukapige makofi. Upanga wako na upige mara mbili, naam, hata mara tatu. Ni upanga wa kuchinja, upanga wa mauaji makuu, ukiwashambulia kutoka kila upande. Ili mioyo ipate kuyeyuka na wanaouawa wawe wengi, nimeweka upanga wa kuchinja kwenye malango yao yote. Lo! Umetengenezwa umetemete kama umeme wa radi, umeshikwa kwa ajili ya kuua. Ee upanga, kata upande wa kuume, kisha upande wa kushoto, mahali popote makali yako yatakapoelekezwa. Mimi nami nitapiga makofi, nayo ghadhabu yangu itapungua. Mimi BWANA nimesema.”