Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 22:1-16

Ezekieli 22:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Ewe mtu! Uko tayari kutoa hukumu, kuuhukumu mji huu wa wauaji? Basi, ujulishe machukizo yake yote. Uambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe ni mji unaowaua watu wako mwenyewe na kujitia unajisi kwa kufanya sanamu za miungu; kwa hiyo wakati wako wa adhabu umewadia. Una hatia kutokana na damu uliyomwaga. Umejifanya najisi kwa sanamu ulizojifanyia. Siku yako ya adhabu umeileta karibu nawe; naam, siku zako zimehesabiwa. Ndio maana nimekufanya udhihakiwe na mataifa na kudharauliwa na nchi zote. Nchi zote za mbali na karibu zitakudhihaki. Umejipatia sifa mbaya na kujaa fujo. “Wakuu wa Israeli walioko kwako, kila mmoja kadiri ya nguvu zake huua watu. Kwako baba na mama wanadharauliwa. Mgeni anayekaa kwako anapokonywa mali yake. Yatima na wajane wanaonewa. Wewe umedharau vyombo vyangu vitakatifu na kuzikufuru sabato zangu. Kwako wamo wanaowasingizia wengine ili wauawe. Wakazi wako hushiriki chakula kilichotolewa kwa miungu milimani. Watu wako wanatenda ufisadi. Kwako wamo watu ambao hulala na wake za baba zao. Huwanajisi wanawake katika siku zao za hedhi. Wengine hufanya machukizo kwa kulala na wake za majirani zao. Wengine hulala na wake za watoto wao, na wengine hulala na dada zao. Huko kwako kuna watu ambao huua kwa malipo. Umepokea riba na kuwalangua wenzako ili kujitajirisha, na kunisahau mimi kabisa! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nimekunja ngumi yangu dhidi yako kwa sababu ya hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo halali na kwa mauaji yaliyofanyika kwako. Je, utaweza kustahimili kuwa hodari siku nitakapopambana nawe? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema na nitayatekeleza hayo. Nitakutawanya kati ya mataifa na kukutupatupa katika nchi nyingine. Nitaukomesha uchafu ulioko kwako. Utajiweka najisi mbele ya mataifa mengine, lakini utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Ezekieli 22:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Na wewe, mwanadamu, je! Utauhukumu, utauhukumu mji huu wa damu? Basi uujulishe machukizo yake yote. Nawe utasema, Bwana MUNGU asema hivi; Mji umwagao damu ndani yake, ili wakati wake upate kuja; mji ufanyao vinyago juu ya nafsi yake, ili ujitie unajisi! Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote. Zilizo karibu, na zilizo mbali nawe, zitakudhihaki, Ewe mchafu, uliyejaa fujo. Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu. Ndani yako wamedharau baba na mama; kati yako wamewatenda wageni udhalimu; ndani yako wamewaonea yatima na mjane. Umevidharau vitu vyangu vitakatifu, umezitia unajisi sabato zangu. Wasingiziaji wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu; na ndani yako wamekula juu ya milima; kati yako wamefanya uasherati. Ndani yako wamefunua uchi wa baba zao; ndani yako wamemfanyia nguvu mwanamke asiye safi wakati wa kutengwa kwake. Na mtu mmoja amefanya chukizo pamoja na mke wa jirani yake; na mtu mwingine amemharibu mke wa mwanawe kwa uasherati; na mtu mwingine ndani yako amemfanyia nguvu dada yake, binti ya babaye. Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU. Basi, tazama, nimeipigia kofi hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo haki, na hiyo damu yako iliyokuwa kati yako. Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, BWANA, nimenena neno hili, tena nitalitenda. Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke. Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Ezekieli 22:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Na wewe, mwanadamu, je! Utauhukumu, utauhukumu mji huu wa damu? Basi uujulishe machukizo yake yote. Nawe utasema, Bwana MUNGU asema hivi; Mji umwagao damu ndani yake, ili wakati wake upate kuja; mji ufanyao vinyago juu ya nafsi yake, ili ujitie unajisi! Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote. Zilizo karibu, na zilizo mbali nawe, zitakudhihaki, Ewe mchafu, uliyejaa fujo. Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu. Ndani yako wamedharau baba na mama; kati yako wamewatenda wageni udhalimu; ndani yako wamewaonea yatima na mjane. Umevidharau vitu vyangu vitakatifu, umezitia unajisi sabato zangu. Wasingiziaji wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu; na ndani yako wamekula juu ya milima; kati yako wamefanya uasherati. Ndani yako wamefunua uchi wa baba zao; ndani yako wamemfanyia nguvu mwanamke asiye safi wakati wa kutengwa kwake. Na mtu mmoja amefanya chukizo pamoja na mke wa jirani yake; na mtu mwingine amemharibu mke wa mwanawe kwa uasherati; na mtu mwingine ndani yako amemfanyia nguvu umbu lake, binti ya babaye. Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU. Basi, tazama, nimeipigia kofi hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo haki, na hiyo damu yako iliyokuwa kati yako. Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, BWANA, nimenena neno hili, tena nitalitenda. Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke. Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Ezekieli 22:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji umwagao damu? Basi uujulishe juu ya matendo yake yote ya machukizo uuambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ee mji ule ujileteao maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu, umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote. Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, Ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia. “ ‘Ona jinsi kila mkuu wa Israeli aliyeko ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu. Ndani yako wamewadharau baba na mama, ndani yako wamewatendea wageni udhalimu na kuwaonea yatima na wajane. Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu. Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za miungu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati. Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa si safi. Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti wa baba yake hasa. Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa jirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema BWANA Mwenyezi. “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi BWANA nimesema na nitalifanya. Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. Ukiisha kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”