Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:1-21

Ezekieli 23:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja; nao walizini huko Misri; walizini wakati wa ujana wao; huko vifua vyao vililemewa, na huko waliyabana matiti ya ubikira wao. Na majina yao, mkubwa aliitwa Ohola, na umbu lake Oholiba; wakawa wangu, wakazaa wana na binti. Na katika hayo majina yao, Samaria ni Ohola, na Yerusalemu ni Oholiba. Na Ohola alifanya mambo ya kikahaba alipokuwa wangu; naye alipenda mno wapenzi wake, Waashuri, jirani zake, waliovikwa samawi, maliwali na mawaziri, wote vijana wa kutamanika, wapanda farasi wakipanda farasi zao. Akawagawia mambo yake ya kikahaba, watu wateule wa Ashuru, wote pia; akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mmoja wa hao aliowapenda. Wala hakuyaacha mambo yake ya kikahaba tangu siku za Misri, kwa maana wakati wa ujana wake walilala naye, wakayabana matiti ya ubikira wake wakamwaga uzinzi wao juu yake. Kwa sababu hiyo nalimtia katika mikono ya wapenzi wake, katika mikono ya Waashuri, aliowapendelea. Na hawa wakaufunua uchi wake, wakatwaa wanawe na binti zake, wakamwua yeye kwa upanga; akawa jina la aibu kati ya wanawake; kwa maana walitoa hukumu juu yake. Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake. Aliwapendelea Waashuri, maliwali na mawaziri, jirani zake, waliovikwa nguo za shani, wapanda farasi wakipanda farasi zao, wote pia vijana wa kutamanika. Nikaona ya kuwa ametiwa unajisi; wote wawili walifuata njia moja. Naye akaongeza uzinzi wake; kwa maana aliona watu waume, ambao sura zao zimeandikwa ukutani, sura za Wakaldayo zilizoandikwa kwa rangi nyekundu; waliofungiwa mikumbuu viunoni mwao, na vilemba vilivyotiwa rangi vichwani mwao; wote wakuu wa kuangaliwa, kwa mfano wa wana wa Babeli katika Ukaldayo, katika nchi ya kuzaliwa kwao. Na mara alipowaona aliwapendelea, akatuma wajumbe kwao hata Ukaldayo. Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao. Basi alifunua uzinzi wake, na kufunua uchi wake; ndipo roho yangu ikafarakana naye, kama ilivyofarakana na umbu lake. Lakini aliongeza uzinzi wake, akikumbuka siku za ujana wake, alipofanya mambo ya kikahaba katika nchi ya Misri. Akawapendelea wapenzi wao, ambao nyama ya mwili wao ni kama nyama ya mwili wa punda, nacho kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. Ndivyo ulivyokumbuka uasherati wa ujana wako, yalipobanwa matiti yako na Wamisri, kwa maziwa ya ujana wako.

Ezekieli 23:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Palikuwa na binti wawili, wote wa mama mmoja. Walipokuwa vijana tu, wakiwa wanakaa kule Misri, wakakubali matiti yao kutomaswa, wakapoteza ubikira wao, wakawa malaya. Yule mkubwa aliitwa Ohola, na yule mdogo Oholiba. Basi, wote wakawa wangu, wakanizalia watoto, wa kiume na wa kike. Basi, Ohola ni Samaria na Oholiba ni Yerusalemu! “Ingawa Ohola alikuwa mke wangu, lakini aliendelea kuwa mzinzi na kuwatamani wapenzi wake wa Ashuru. Hao walikuwa askari, wamevalia sare za rangi ya zambarau, watawala na makamanda. Wote walikuwa vijana wa kuvutia na wapandafarasi hodari. Ohola alifanya zinaa na hao maofisa wote wa vyeo vya juu wa Ashuru naye akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mwanamume wake aliyemtamani. Aliendelea na uzinzi wake aliouanza kule Misri wakati huo, akiwa bado kijana, wanaume walivunja ubikira wake na kuzitimiza tamaa zao kwake. Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa Waashuru wapenzi wake, ambao aliwatamani sana. Hao walimvua mavazi yake na kumwacha uchi. Waliwakamata watoto wake, naye mwenyewe wakamuua kwa upanga. Adhabu hiyo aliyopata ikawa fundisho kwa wanawake wengine. “Oholiba dada yake, aliona jambo hilo, lakini akawa amepotoka kuliko yeye katika tamaa yake na uzinzi wake uliokuwa mbaya kuliko wa dada yake. Aliwatamani sana Waashuru: Wakuu wa mikoa, makamanda, wanajeshi waliovaa sare zao za kijeshi, wapandafarasi hodari, wote wakiwa vijana wa kuvutia. Nilimtambua kuwa najisi. Ama kweli wote wawili walikuwa na tabia hiyo moja. Lakini Oholiba alizidisha uzinzi wake; akapendezwa na picha za Wakaldayo zilizochorwa ukutani, zimetiwa rangi nyekundu, mikanda viunoni, vilemba vikubwa vichwani; hizo zote zilifanana na maofisa, naam, picha ya Wababuloni, wakazi wa nchi ya Wakaldayo. Alipoziona picha hizo, mara akashikwa na tamaa, akatuma wajumbe kwenda Ukaldayo. Basi, Wababuloni wakaja kulala naye. Wakamtia najisi kwa tamaa zao. Alipokwisha tiwa najisi, akajitenga nao. Alipoendelea na uzinzi wake na kufunua uchi wake, mimi nilimwacha kama nilivyomwacha dada yake. Hata hivyo, akazidisha uzinzi wake akifanya kama wakati wa ujana wake alipofanya uzinzi kule Misri. Aliwatamani sana wanaume wenye tamaa mbaya kama ya punda na nguvu nyingi za uzazi kama farasi dume.” “Oholiba aliutamani uchafu wake wa ujana alipokuwa Misri, ambako Wamisri walivunja ubikira wake, na kuyatomasa matiti yake machanga.

Ezekieli 23:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja; nao walizini huko Misri; walizini wakati wa ujana wao; huko vifua vyao vilishikwashikwa, na matiti yao yakatomaswa wakapoteza ubikira wao. Na majina yao, mkubwa aliitwa Ohola, na dada yake Oholiba; wakawa wangu, wakazaa watoto wa kiume na wa kike. Na katika hayo majina yao, Samaria ni Ohola, na Yerusalemu ni Oholiba. Na Ohola alifanya mambo ya kikahaba alipokuwa wangu; naye alipenda mno wapenzi wake, Waashuri, jirani zake, waliovikwa mavazi ya samawati, watawala na mawaziri, wote vijana wa kutamanika, wapanda farasi wakipanda farasi wao. Akawagawia mambo yake ya kikahaba, watu wateule wa Ashuru, wote pia; akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mmoja wa hao aliowapenda. Wala hakuyaacha mambo yake ya kikahaba tangu siku za Misri, kwa maana wakati wa ujana wake walilala naye, wakayabana matiti ya ubikira wake wakamwaga uzinzi wao juu yake. Kwa sababu hiyo nilimtia katika mikono ya wapenzi wake, katika mikono ya Waashuri, aliowapendelea. Na hawa wakaufunua uchi wake, wakatwaa wanawe na binti zake, wakamwua yeye kwa upanga; akawa jina la aibu kati ya wanawake; kwa maana walitoa hukumu juu yake. Na dada yake, Oholiba, akayaona hayo lakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa dada yake. Aliwapendelea Waashuri, watawala na mawaziri, jirani zake, waliovikwa nguo za shani, wapanda farasi wakipanda farasi wao, wote pia vijana wa kutamanika. Nikaona ya kuwa ametiwa unajisi; wote wawili walifuata njia moja. Naye akaongeza uzinzi wake; kwa maana aliona wanaume, ambao sura zao zimeandikwa ukutani, sura za Wakaldayo zilizoandikwa kwa rangi nyekundu; waliofungiwa mikumbuu viunoni mwao, na vilemba vilivyotiwa rangi vichwani mwao; wote wakuu wa kuangaliwa, kwa mfano wa wana wa Babeli katika Ukaldayo, katika nchi ya kuzaliwa kwao. Na mara alipowaona aliwapendelea, akatuma wajumbe kwao hata Ukaldayo. Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao. Basi alipoendelea na ukahaba wake waziwazi, na kufunua uchi wake; ndipo roho yangu ikafarakana naye, kama ilivyofarakana na dada yake. Lakini aliongeza uzinzi wake, akikumbuka siku za ujana wake, alipofanya mambo ya kikahaba katika nchi ya Misri. Akawapendelea wapenzi wao, ambao nyama ya mwili wao ni kama nyama ya mwili wa punda, nacho kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. Ndivyo ulivyokumbuka uasherati wa ujana wako, yalipobanwa matiti yako na Wamisri, kwa maziwa ya ujana wako.

Ezekieli 23:1-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, walikuwepo wanawake wawili, binti wa mama mmoja. Wakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa huko na wakapoteza ubikira wao. Mkubwa aliitwa Ohola na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa wavulana na msichana. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu. “Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru, waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi. Akafanya ukahaba na wasomi wote wa Ashuru, na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani. Hakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati ambapo tangu ujana wake wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake. “Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani. Wakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukua wanawe na binti zake, naye wakamuua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake na adhabu ikatolewa dhidi yake. “Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola dada yake. Yeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia. Nikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja. “Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo waliovalia nguo nyekundu, wakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Babeli wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo. Mara tu alipowaona, aliwatamani, akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo. Ndipo hao Wababeli wakaja kwake kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi, akawaacha kwa kuwachukia. Alipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonyesha hadharani uchi wake, nilimwacha kwa kumchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake. Lakini akazidisha zaidi ukahaba wake alipozikumbuka siku zake za ujana, alipokuwa kahaba huko Misri. Huko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda, na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. Hivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri, kifua chako kilipokumbatiwa, na walipokutomasa kwa sababu ya matiti yako machanga.