Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 24:1-14

Ezekieli 24:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi, neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, weka kumbukumbu ya tarehe hii, tarehe hii hasa, kwa kuwa mfalme wa Babeli ameuzingira mji wa Yerusalemu kwa jeshi siku hii ya leo. Iambie nyumba hii ya kuasi fumbo, na uwaambie, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Teleka sufuria jikoni; iteleke na umimine maji ndani yake, Weka vipande vya nyama ndani yake, vipande vyote vizuri, vya paja na vya bega. Ijaze hiyo sufuria kwa mifupa hii mizuri; chagua yule aliye bora wa kundi la kondoo. Panga kuni chini ya sufuria kwa ajili ya mifupa; chochea mpaka ichemke na uitokose hiyo mifupa ndani yake. “ ‘Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Ole wa mji umwagao damu, ole wa sufuria ambayo sasa ina ukoko ndani yake, ambayo ukoko wake hautoki. Kipakue kipande baada ya kipande, bila kuvipigia kura. “ ‘Kwa kuwa damu aliyoimwaga ipo katikati yake: huyo mwanamke aliimwaga juu ya mwamba ulio wazi; hakuimwaga kwenye ardhi, ambako vumbi lingeifunika. Kuchochea ghadhabu na kulipiza kisasi, nimemwaga damu yake juu ya mwamba ulio wazi, ili isifunikwe. “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Ole wa mji umwagao damu! Mimi nami nitalundikia kuni nyingi. Kwa hiyo lundika kuni na uwashe moto. Pika hiyo nyama vizuri, changanya viungo ndani yake, na uiache mifupa iungue kwenye moto. Kisha teleka sufuria tupu kwenye makaa mpaka iwe na moto sana na shaba yake ingʼae, ili uchafu wake upate kuyeyuka na ukoko wake upate kuungua na kuondoka. Imezuia juhudi zote, ukoko wake mwingi haujaondoka, hata ikiwa ni kwa moto. “ ‘Sasa uchafu wako ni uasherati wako. Kwa sababu nilijaribu kukutakasa lakini haikuwezekana kutakaswa kutoka kwenye huo uchafu wako, hutatakasika tena mpaka ghadhabu yangu dhidi yako iwe imepungua. “ ‘Mimi BWANA nimesema, wakati umewadia wa mimi kutenda. Mimi sitazuia, mimi sitaona huruma wala sitapunguza hasira yangu, Utahukumiwa sawasawa na mwenendo na matendo yako, asema BWANA Mwenyezi.’ ”

Ezekieli 24:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo siku ya kumi, mwezi wa kumi, mwaka wa tisa tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Andika tarehe ya siku ya leo, maana hii ni siku ambapo mfalme wa Babuloni anaanza kuuzingira mji wa Yerusalemu. Wape mfano hao watu wangu waasi na kuwaambia kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kiweke chungu juu ya meko, ukakijaze maji pia. Tia humo vipande vya nyama, vipande vizuri vya mapaja na mabega. Kijaze pia mifupa mizuri. Tumia nyama nzuri ya kondoo, panga kuni chini ya chungu, chemsha vipande vya nyama na mifupa, vyote uvichemshe vizuri. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mji huo ni kama chungu chenye kutu, ambacho kutu yake haiwezi kutoka! Vipande vya nyama ndani yake hutolewa kimojakimoja bila kuchaguliwa. Mauaji yamo humo mjini; damu yenyewe haikumwagwa udongoni ifunikwe na vumbi, ila ilimwagwa mwambani. Damu hiyo nimeiacha huko mwambani ili isifunikwe, nipate kuamsha ghadhabu yangu na kulipiza kisasi. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wake mji wa mauaji! Mimi nitarundika rundo kubwa la kuni. Nitaleta magogo ya kuni na kuwasha moto. Nitachemsha nyama vizuri sana. Nitachemsha na kukausha mchuzi, na mifupa nitaiunguza! Hicho chungu kitupu nitakiweka juu ya makaa kipate moto sana, shaba yake ipate moto, uchafu wake uyeyushwe na kutu iunguzwe. Lakini najisumbua bure; kutu yake nene haitoki hata kwa moto. Ewe Yerusalemu, matendo yako machafu yamekutia unajisi. Ingawa nilijaribu kuutakasa, wenyewe ulibaki najisi. Basi, hutatakasika tena mpaka nitakapoitosheleza hasira yangu juu yako. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Jambo hilo litakamilika; mimi nitalitenda. Sitaghairi jambo hilo wala kukuonea huruma. Nitakuadhibu kulingana na mwenendo na matendo yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Ezekieli 24:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena, katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, liandike jina la siku hii, naam, la siku ii hii; mfalme wa Babeli ameuzingira Yerusalemu siku ii hii. Ukawatungie mithali nyumba ya kuasi, ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Teleka sufuria, liteleke; ukatie maji ndani yake; vikusanye vipande vyake ndani yake, naam, kila kipande chema, paja na bega; lijaze mifupa iliyochaguliwa. Uwatwae wateule wa kundi la kondoo, ukafanye chungu ya mifupa chini yake; ukalitokose sana; naam, mifupa yake itokoswe ndani yake. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Hilo sufuria ambalo kutu yake i ndani yake, ambalo kutu yake haikulitoka; litoe kipande kipande; hapana kura iliyoanguka juu yake. Maana damu yake imo ndani yake; aliiweka juu ya jabali lililo wazi; hakuimwaga juu ya nchi, apate kuifunika kwa mavumbi; ili ipandishe ghadhabu ya kulipa kisasi, nimeiweka damu yake juu ya jabali lililo wazi, isipate kufunikwa. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Mimi nami nitaiongeza chungu. Tia kuni nyingi, uchochee moto, itokose nyama sana, fanyiza mchuzi mzito, mifupa ikateketee. Kisha litie juu ya makaa yake, tupu, lipate moto, na shaba yake iteketee, uchafu wake uyeyushwe, na kutu yake iteketee. Amejidhoofisha kwa taabu, lakini kutu yake nyingi haikumtoka; kutu yake haitoki kwa moto. Katika uchafu wako mna uasherati, kwa maana nimekusafisha, ila wewe hukusafika; hutasafishwa tena uchafu wako ukutoke, hadi nitakapokuwa nimeituliza hasira yangu kwako. Mimi, BWANA, nimenena neno hili, nalo litakuwa; nami nitalifanya; sitaachilia, wala sitahurumia, wala sitajuta; kulingana na njia zako, na kulingana na matendo yako, ndivyo watakavyokuhukumu, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 24:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena, katika mwaka wa kenda, mwezi wa kumi, siku ya kumi ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, liandike jina la siku hii, naam, la siku ii hii; mfalme wa Babeli ameukaribia Yerusalemu siku iyo hiyo. Ukawatungie mithali nyumba ya kuasi, ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Teleka sufuria, liteleke; ukatie maji ndani yake; vikusanye vipande vyake ndani yake, naam, kila kipande chema, paja na bega; lijaze mifupa iliyochaguliwa. Uwatwae wateule wa kundi la kondoo, ukafanye chungu ya mifupa chini yake; ukalitokose sana; naam, mifupa yake itokoswe ndani yake. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Hilo sufuria ambalo kutu yake i ndani yake, ambalo kutu yake haikulitoka; litoe kipande kipande; hapana kura iliyoanguka juu yake. Maana damu yake imo ndani yake; aliiweka juu ya jabali lililo wazi; hakuimwaga juu ya nchi, apate kuifunika kwa mavumbi; ili ipandishe ghadhabu ya kulipa kisasi, nimeiweka damu yake juu ya jabali lililo wazi, isipate kufunikwa. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Mimi nami nitaiongeza chungu. Tia kuni nyingi, uchochee moto, itokose nyama sana, fanyiza mchuzi mzito, mifupa ikateketee. Kisha litie juu ya makaa yake, tupu, lipate moto, na shaba yake iteketee, uchafu wake uyeyushwe, na kutu yake iteketee. Amejidhoofisha kwa taabu, lakini kutu yake nyingi haikumtoka; kutu yake haitoki kwa moto. Katika uchafu wako mna uasherati, kwa maana nimekusafisha, ila wewe hukusafika; hutasafishwa tena uchafu wako ukutoke, hata nitakapokuwa nimeituliza hasira yangu kwako. Mimi, BWANA, nimenena neno hili, nalo litakuwa; nami nitalifanya; sitaachilia, wala sitahurumia, wala sitajuta; sawasawa na njia zako, na sawasawa na matendo yako, ndivyo watakavyokuhukumu, asema Bwana MUNGU.