Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 4:1-17

Ezekieli 4:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

“Wewe mtu, chukua tofali, uliweke mbele yako; kisha chora juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu. Onesha kuwa umezingirwa. Chora ngome dhidi yake na maboma kandokando yake, makambi ya askari kandokando yake, na magogo ya kuubomolea. Kisha, chukua bamba la chuma ulisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na mji. Kisha uelekee mji huo unaozingirwa, uoneshe kana kwamba unazingirwa. Fanya alama ya kuuzingira. Hii itakuwa ishara kwa taifa la Israeli. “Kisha, nenda ukalale kwa upande wako wa kushoto. Muda wote utakapokaa katika hali hiyo utabeba uovu wa Waisraeli kama mzigo mzito. Nimekupangia muda wa siku 390 muda ambao ni sawa na miaka ya adhabu yao. Siku moja ni sawa na mwaka mmoja. Utabeba adhabu ya Waisraeli. Utakapotimiza siku hizo, utalala kwa upande wa kulia, na hapo utabeba adhabu ya watu wa Yuda kwa muda wa siku arubaini; nimekupangia siku moja kuwa sawa na mwaka mmoja. “Kisha, utauelekea mji wa Yerusalemu uliozingirwa na kuunyoshea mkono mtupu na kutabiri dhidi yake. Nitakufunga kamba ili usiweze kugeuka toka upande mmoja hadi upande mwingine, mpaka hapo kuzingirwa kwa Yerusalemu kutakapomalizika. “Chukua ngano, shayiri, maharagwe, choroko, mtama na mawele, uvitie vyote katika chombo kimoja, ujitengenezee mkate. Mkate huo ndio utakaokuwa chakula chako wakati unapolala kwa upande mmoja, siku zote 390. Chakula utakachokula lazima kipimwe, nacho kitakuwa gramu 230 kwa siku; nawe utakula mara moja tu kwa siku. Maji nayo utakunywa kwa kipimo: Vikombe viwili, mara moja kwa siku. Utachukua mavi ya mtu, uwashe moto, uoke mkate, na kuula mbele ya watu.” Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Hivyo ndivyo Waisraeli watakavyokula mkate wao unajisi wakiwa kati ya mataifa ninakowapeleka.” Ndipo nikamwambia, “Ee, Bwana Mwenyezi-Mungu, kamwe sijajitia najisi kwa kula kilichokufa chenyewe au kilichouawa na mnyama wa porini, wala sijapata kuonja nyama ya mnyama najisi tangu ujana wangu.” Kisha akaniambia, “Basi, nakuruhusu utumie mavi ya ng'ombe badala ya mavi ya mtu ili kuokea mkate wako.” Tena akaniambia, “Wewe mtu, mimi nitaharibu akiba ya chakula mjini Yerusalemu; wakazi wake watakula chakula watakachopimiwa kwa hofu. Watakunywa maji watakayopimiwa kwa kufadhaika. Nitafanya hivyo ili wakose chakula na maji, na kila mmoja atamwangalia mwenzake kwa kufadhaika; nao watadhoofika kwa adhabu yao.”

Shirikisha
Soma Ezekieli 4

Ezekieli 4:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wewe nawe, mwanadamu, jipatie tofali uliweke mbele yako, kisha, chora juu yake mfano wa mji, yaani, Yerusalemu; ukauhusuru, ukajenge ngome juu yake, na kufanya boma juu yake; ukaweke makambi juu yake, na kuweka magogo ya kuubomoa yauzunguke pande zote. Kisha ukajipatie bamba la chuma, ukalisimamishe liwe ukuta wa chuma kati ya wewe na mji huo; ukaelekeze uso wako juu yake, nao utahusuriwa, nawe utauhusuru. Hili litakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli. Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao. Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kulia, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arubaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia. Nawe utauelekeza uso wako, uelekee kuzingirwa kwa Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake. Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za kuzingirwa kwako. Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula. Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake. Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake. Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu. BWANA akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na wanyama; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu. Ndipo akaniambia, Tazama, nimekupa mashonde ya ng'ombe badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo. Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa hofu; wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao.

Shirikisha
Soma Ezekieli 4

Ezekieli 4:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wewe nawe, mwanadamu, jipatie tofali uliweke mbele yako, kisha, chora juu yake mfano wa mji, yaani, Yerusalemu; ukauhusuru, ukajenge ngome juu yake, na kufanya boma juu yake; ukaweke makambi juu yake, na kuweka magogo ya kuubomoa yauzunguke pande zote. Kisha ukajipatie bamba la chuma, ukalisimamishe liwe ukuta wa chuma kati ya wewe na mji huo; ukaelekeze uso wako juu yake, nao utahusuriwa, nawe utauhusuru. Hili litakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli. Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao. Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia. Nawe utauelekeza uso wako, uelekee mazingiwa ya Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake. Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za mazingiwa yako. Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula. Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake. Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake. Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu. BWANA akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na hayawani; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu. Ndipo akaniambia, Tazama, nimekupa mashonde ya ng’ombe badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo. Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa kushangaa; wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao.

Shirikisha
Soma Ezekieli 4

Ezekieli 4:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Mwanadamu, sasa chukua tofali, uliweke mbele yako na uchore juu yake ramani ya mji wa Yerusalemu. Kisha uuzingire: Simamisha askari dhidi yake kuuzunguka, uzunguke kwa majeshi, weka kambi dhidi yake pande zote pamoja na magogo ya kubomolea boma vitani. Kisha chukua bamba la chuma, ukalisimamishe liwe kama ukuta wa chuma kati yako na huo mji, nawe uuelekeze uso wako. Huo mji utakuwa katika hali ya kuzingirwa, nawe utauzingira. Hii itakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli. “Kisha ulale kwa upande wako wa kushoto na uweke dhambi za nyumba ya Israeli juu yake. Utazibeba dhambi zao kwa idadi ya siku utakazolala kwa huo upande mmoja. Nimekupangia idadi ya siku kama miaka ya dhambi yao. Kwa hiyo kwa siku 390 utabeba dhambi za nyumba ya Israeli. “Baada ya kumaliza hili, lala chini tena, wakati huu ulale chini kwa upande wa kuume, uchukue dhambi za nyumba ya Yuda. Nimekupangia siku arobaini, siku moja kwa kila mwaka mmoja. Geuza uso wako uelekeze kwenye kuzingirwa kwa Yerusalemu na mkono wako ambao haukuvikwa nguo tabiri dhidi yake. Nitakufunga kwa kamba ili usiweze kugeuka kutoka upande mmoja hadi upande mwingine, mpaka hapo utakapokuwa umetimiza siku za kuzingirwa kwako. “Chukua ngano na shayiri, maharagwe na dengu, mtama na mawele, uviweke na kuvihifadhi vyote kwenye gudulia la kuhifadhia, na uvitumie kujitengenezea mkate. Utaula mkate huo kwa hizo siku 390 utakazokuwa umelala kwa upande mmoja. Pima shekeli ishirini za chakula utakachokula kwa kila siku, nawe utakula kwa wakati uliopangwa. Pia pima maji moja ya sita ya hini, nawe utakunywa kwa wakati uliopangwa. Nawe utakula chakula kama vile ambavyo ungekula mkate wa shayiri, uoke mkate mbele ya macho ya watu, ukitumia kinyesi cha mwanadamu.” BWANA akasema, “Hivi ndivyo watu wa Israeli watakavyokula chakula kilicho najisi miongoni mwa mataifa ninakowapeleka.” Ndipo nikasema, “Sivyo BWANA Mwenyezi! Kamwe mimi sijajitia unajisi. Tangu ujana wangu hadi sasa sijala kamwe kitu chochote kilichokufa au kilichoraruliwa na wanyama wa mwituni. Hakuna nyama yeyote najisi iliyoingia kinywani mwangu.” Akasema, “Vema sana, basi nitakuruhusu uoke mkate wako kwa kutumia kinyesi cha ngʼombe badala ya kinyesi cha mwanadamu.” Ndipo Mungu akaniambia, “Mwanadamu, mimi nitakatilia mbali upatikanaji wa chakula katika Yerusalemu. Watu watakula chakula cha kupimwa kwa wasiwasi pamoja na maji ya kupimiwa kwa kukata tamaa, kwa kuwa chakula na maji vitakuwa adimu. Watastajabiana kila mmoja, nao watadhoofika kwa sababu ya dhambi yao.

Shirikisha
Soma Ezekieli 4