Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 41:5-26

Ezekieli 41:5-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Yule mtu aliupima unene wa ukuta wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nao ulikuwa mita tatu. Kulikuwa na mfululizo wa vyumba vidogovidogo kuizunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu, vyenye upana wa mita mbili. Vyumba hivi, vilikuwa katika majengo ya ghorofa tatu, na kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Ukuta wa nje wa hekalu kila kwenye ghorofa ulikuwa mwembamba kuliko ule wa ghorofa ya chini, ili vile vyumba viwe imara bila ya kuutegemea ukuta wa hekalu. Kwa upande, zile kuta za hekalu zikitazamwa kutokea nje, zilionekana kuwa na unene uleule toka chini hadi juu. Mkabala na ukuta wa nje wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, nje ya vyumba, kulikuwa na ngazi mbili, ambazo zilifanya iwe rahisi kwenda juu kutokea ghorofa ya chini hadi ile ya juu. Kisha, nikaona kuwa hekalu lilikuwa na sakafu iliyonyanyuliwa kulizunguka, nayo ilikuwa ndio msingi wa zile ghorofa tatu mkabala na hekalu, kimo cha msingi wa ghorofa hizo ulikuwa sawa na ule ufito wa kupimia, mita tatu. Unene wa ukuta wa nje wa vyumba vya ndani ulikuwa mita mbili u nusu. Nafasi wazi kati ya vyumba vya pembeni mkabala na hekalu na vyumba vya walinzi vilikuwa na upana wa mita 10, kuzunguka hekalu. Kulikuwa na milango kwenye vyumba vya pembeni kutokea kwenye uwanja, mmoja upande wa kaskazini na mwingine upande wa kusini. Na msingi uliounganishwa na uwanja ulikuwa na upana wa mita 2.5. Mwishoni kabisa mwa uwanja, upande wa magharibi kulikuwa na jengo lenye urefu wa mita 45 na upana wa mita 35. Kuta zake zilikuwa na unene wa mita 2.5. Yule mtu akapima upande wa nje wa hekalu nao ulikuwa na urefu wa mita 50. Tokea nyuma ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kupitia ile nafasi ya kupitia, hadi mwisho wake, upande wa magharibi, umbali wake ulikuwa pia mita 50. Urefu mbele ya hekalu tangu upande huu hadi upande huu ukichanganya na ile nafasi wazi, ulikuwa pia mita 50. Yule mtu akapima urefu wa jengo hadi magharibi pamoja na mabaraza yake pande zake zote, nalo lilikuwa na urefu wa mita 50. Chumba cha kuingilia hekaluni, mahali patakatifu, na mahali patakatifu kabisa, vyote vilipambwa kwa mbao tangu sakafuni hadi kwenye madirisha. Madirisha haya yangeweza kufunikwa. Mpaka kwenye nafasi juu ya mlango hata kwenye chumba cha ndani na nje yake, pia juu ya kuta ndani ya chumba cha ndani na kwenye ukumbi palikuwapo na michoro iliyofanana na mitende na picha za viumbe wenye mabawa. Kila baada ya mtende kulichorwa picha ya kiumbe chenye mabawa kukizunguka chumba chote. Kila kiumbe alikuwa na nyuso mbili: Uso wa mwanadamu ulioelekea kwenye mtende upande mmoja na uso wa simba ulioelekea kwenye mtende wa upande mwingine. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwenye nyumba nzima, tangu sakafu hadi juu ya milango palichorwa viumbe wenye mabawa na mitende. Miimo ya mahali patakatifu ilikuwa ya mraba. Mbele ya mlango wa kuingilia mahali patakatifu kabisa kulikuwa na kitu kilichoonekana kama madhabahu ya mbao. Kimo chake kilikuwa nusu mita na upana wa mita moja. Pembe zake, tako lake, na pande zake zote zilikuwa zimetengenezwa kwa mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ndiyo meza inayokaa mbele ya Mwenyezi-Mungu.” Kulikuwako na mlango wa tarabe wa kuingia kwenye ukumbi wa hekalu na mlango wa tarabe wa kuingia mahali patakatifu kabisa. Milango hiyo ilikuwa ya tarabe, kwa hiyo kila mlango uliweza kufunguka katikati. Kwenye mlango wa kuingilia ukumbi kulichorwa viumbe vyenye mabawa na mitende, kama ilivyokuwa kwenye kuta. Na kulikuwa na kifuniko cha ubao kikifunika mlango kwa nje kwenye sehemu ya kuingilia ndani. Pembeni mwa chumba hiki, kulikuwa na madirisha madogo na kuta zilipambwa kwa michoro ya mitende.

Ezekieli 41:5-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni, dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote. Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na ghorofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta wa nyumba. Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hadi juu; basi hupanda juu toka chumba cha chini hadi chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati. Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita. Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya nyumba, na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote. Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote. Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu wake dhiraa tisini. Basi akaipima nyumba, urefu wake dhiraa mia moja; na mahali pale palipotengeka na jengo lile, pamoja na kuta zake, urefu wake dhiraa mia moja; tena upana wa uso wa nyumba, na wa mahali palipotengeka upande wa mashariki, dhiraa mia. Akaupima urefu wa jengo lile lililokabili mahali palipotengeka, palipokuwa nyuma yake, na baraza zake upande huu na upande huu, dhiraa mia moja; na hekalu la ndani, na kumbi za ua; na vizingiti, na madirisha yaliyofungwa, na baraza za pande zote za ghorofa zile tatu, zilizokikabili kizingiti, zilitiwa mabamba ya mti pande zote; na toka chini hadi madirishani; (nayo madirisha yamefunikwa); na mpaka juu ya mlango hata nyumba ya ndani, na nje, na juu ya kuta zote pande zote, katika nyumba ya ndani, na ya nje, kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili; basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwanasimba kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote. Toka chini hadi juu ya mlango makerubi yamefanyika, na mitende, na vivi hivi ukuta wa hekalu. Na hilo hekalu, miimo ya milango yake ilikuwa ya miraba; na mbele ya patakatifu kuonekana kwake palionekana kama hapo kwanza. Madhabahu ilikuwa ni ya miti, kimo chake dhiraa tatu, na urefu wake dhiraa mbili; na pembe zake, na msingi wake, na kuta zake zilikuwa za miti; akaniambia, Hii ndiyo meza iliyo mbele za BWANA. Nalo hekalu na patakatifu palikuwa na milango miwili. Na milango hiyo, kila mmoja ulikuwa na mbao mbili; mbao mbili zigeukazo; mbao mbili za mlango mmoja, na mbao mbili za mlango wa pili. Na milango ya hekalu ilitengenezwa makerubi na mitende vile vile, kama zile kuta zilivyotengenezwa; tena palikuwa na boriti nene juu ya uso wa ukumbi, nje. Tena palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na mitende, upande huu na upande huu, katika pande za ukumbi; ndiyo habari ya vyumba vya mbavuni vya nyumba hiyo, na vya boriti zile nene.

Ezekieli 41:5-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni, dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote. Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na orofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta wa nyumba. Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hata juu; basi hupanda juu toka chumba cha chini hata chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati. Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita. Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya nyumba, na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote. Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote. Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu wake dhiraa tisini. Basi akaipima nyumba, urefu wake dhiraa mia; na mahali pale palipotengeka na jengo lile, pamoja na kuta zake, urefu wake dhiraa mia; tena upana wa uso wa nyumba, na wa mahali palipotengeka upande wa mashariki, dhiraa mia. Akaupima urefu wa jengo lile lililokabili mahali palipotengeka, palipokuwa nyuma yake, na baraza zake upande huu na upande huu, dhiraa mia; na hekalu la ndani, na kumbi za ua; na vizingiti, na madirisha yaliyofungwa, na baraza za pande zote za orofa zile tatu, zilizokikabili kizingiti, zilitiwa mabamba ya mti pande zote; na toka chini hata madirishani; (nayo madirisha yamefunikwa); na mpaka juu ya mlango hata nyumba ya ndani, na nje, na juu ya kuta zote pande zote, katika nyumba ya ndani, na ya nje, kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili; basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwana-simba kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote. Toka chini hata juu ya mlango makerubi yamefanyika, na mitende, na vivi hivi ukuta wa hekalu. Na hilo hekalu, miimo ya milango yake ilikuwa ya miraba; na mbele ya patakatifu kuonekana kwake palionekana kama hapo kwanza. Madhabahu ilikuwa ni ya miti, kimo chake dhiraa tatu, na urefu wake dhiraa mbili; na pembe zake, na msingi wake, na kuta zake zilikuwa za miti; akaniambia, Hii ndiyo meza iliyo mbele za BWANA. Nalo hekalu na patakatifu palikuwa na milango miwili. Na milango hiyo, kila mmoja ulikuwa na mbao mbili; mbao mbili zigeukazo; mbao mbili za mlango mmoja, na mbao mbili za mlango wa pili. Na milango ya hekalu ilifanyiziwa makerubi na mitende vile vile, kama zile kuta zilivyofanyiziwa; tena palikuwa na boriti nene juu ya uso wa ukumbi, nje. Tena palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na mitende, upande huu na upande huu, katika pande za ukumbi; ndiyo habari ya vyumba vya mbavuni vya nyumba hiyo, na vya boriti zile nene.

Ezekieli 41:5-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha akapima ukuta wa Hekalu, nao ulikuwa na unene wa dhiraa sita, na kila chumba cha pembeni kuzunguka Hekalu kilikuwa na upana wa dhiraa nne. Vyumba vya pembeni vilikuwa na ghorofa tatu, kimoja juu ya kingine, kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Kulikuwa na boriti katika ukuta wote wa Hekalu ili kuimarisha vyumba vya pembeni, kwa hiyo boriti hizo hazikushikamanishwa kwenye ukuta wa Hekalu. Vyumba vya pembeni vilivyozunguka Hekalu vilizidi kupanuka kulingana na sakafu zilivyokwenda juu. Ujenzi uliozunguka Hekalu ulijengwa kukwea juu, kwa hiyo vyumba vilipanuka kwa kadiri ya kila kimoja kilivyokwenda juu. Ngazi za kupandia zilianzia sakafu ya chini hadi sakafu ya juu kabisa kwa kupitia sakafu ya kati. Nikaona pia kuwa Hekalu lilikuwa na kitako kilichoinuliwa pande zote, huu ulikuwa ndio msingi wa vile vyumba vya pembeni ambao ulikuwa na urefu wa ule ufito mmoja wa kupimia, yaani, dhiraa ndefu sita. Ukuta wa nje wa vyumba vya pembeni ulikuwa na unene wa dhiraa tano. Eneo la wazi katikati ya vyumba vya pembeni vya Hekalu na vyumba vya makuhani lilikuwa na upana wa dhiraa ishirini kuzunguka Hekalu pande zote. Kulikuwa na maingilio kwenye vyumba vya pembeni kutokea eneo lililo wazi, moja upande wa kaskazini na lingine upande wa kusini, nao msingi uliounganisha lile eneo la wazi ulikuwa na upana wa dhiraa tano ukilizunguka lote. Jengo lililoelekeana na ua wa Hekalu upande wa magharibi lilikuwa na upana wa dhiraa sabini. Ukuta wa jengo hilo ulikuwa na unene wa dhiraa tano, kulizunguka lote, urefu ulikuwa wa dhiraa tisini. Kisha akapima Hekalu, lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na ua wa Hekalu na jengo pamoja na kuta zake vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja pia. Upana wa ua wa Hekalu upande wa mashariki, pamoja na upande wa mbele wa Hekalu ulikuwa dhiraa mia moja. Kisha akapima urefu wa jengo linaloelekeana na ua upande wa nyuma wa Hekalu, pamoja na vyumba vyake kila upande, ilikuwa dhiraa mia moja. Sehemu takatifu ya nje, sehemu takatifu ya ndani, pamoja na baraza inayoelekeana na ukumbi, pamoja na vizingiti, madirisha membamba na vyumba vyote vitatu, kila kimoja pamoja na kizingiti vilifunikwa kwa mbao. Sakafu, ukuta mpaka kwenye madirisha na madirisha yenyewe vilifunikwa kwa mbao. Katika nafasi iliyokuwa juu ya upande wa nje wa ingilio la sehemu takatifu ya ndani, na katika kuta zilizozunguka sehemu takatifu ya ndani na sehemu takatifu ya nje, kwa nafasi zilizo sawa, kulinakshiwa makerubi na miti ya mitende. Miti ya mitende ilikuwa kati ya kerubi na kerubi. Kila kerubi alikuwa na nyuso mbili: upande mmoja uso wa mwanadamu kuelekea mti wa mtende na upande mwingine uso wa simba ukielekea mti mwingine wa mtende. Ilinakshiwa kuzunguka Hekalu lote. Kuanzia sakafu mpaka eneo lililo juu ya ingilio, palinakshiwa makerubi na miti ya mitende pamoja na kwenye ukuta wa nje wa patakatifu. Mahali patakatifu pa nje palikuwa na miimo ya mlango uliokuwa mraba na ule uliokuwa katika Patakatifu Pa Patakatifu ulikuwa unafanana na huo mwingine. Kulikuwa na madhabahu ya mbao kimo chake dhiraa tatu na ilikuwa dhiraa mbili mraba pande zote, tako lake na pande zake zilikuwa za mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ni meza ambayo iko mbele za BWANA.” Mahali patakatifu pa nje na Patakatifu Pa Patakatifu zilikuwa na milango miwili. Kila mlango ulikuwa na vipande viwili, vipande viwili vilivyoshikwa na bawaba vyenye kufunguka kwa kila mlango. Juu ya hiyo milango ya Patakatifu palinakshiwa makerubi na miti ya mitende kama yale yaliyonakshiwa kwenye kuta, na kulikuwa na ubao ulioningʼinia mbele ya baraza kwa nje. Katika kuta za pembeni za ukumbi kulikuwa na madirisha membamba yaliyonakshiwa miti ya mitende kila upande. Vyumba vya pembeni vya Hekalu pia vilikuwa vimefunikwa kwa mbao.